BODI YA DAWASCO YARIDHISHWA NA UWEKEZAJI SEKTA YA MAJI

Mtendaji Mkuu wa Dawasco Mhandisi Cprian Luhemeja akitoa ufafanuzi kwa Bodi mpya ya Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASCO).
**
Bodi mpya ya Shirika la Majisafi na Majitaka jijini Dar es Salaam (DAWASCO),leo imefanya ziara katika mitambo ya uzalishaji Maji ya Ruvu juu na Ruvu chini iliyopo Mkoa wa Pwani ambapo imeridhishwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika sekta ya Maji.

Bodi hiyo imeshuhudia uwekezaji mkubwa kwenye miradi hiyo, na kuridhika na kazi inayofanywa na shirika hilo ambapo waliweza kujihakikishia kuwa hadi kufikia 2020 tatizo la Maji linawezakwisha katika Miji mbalimbali nchini hususani katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kutokana na kuwa na Mitambo ya Kisasa na yenye uwezo mkubwa wa kuhudumia mikoa hiyo.

Akizungumza mara baada ya kuhitimisha ziara hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya DAWASCO, Prof. Tolly Mbwete alisema kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kujionea namna ambavyo serikali imejikita katika kuhakikisha inamaliza tatizo la Maji lililopo nchini na linamtua mama ndoo ya Maji Kichwani.

Prof. Tolly alipongeza jitihada zilizofanywa na serikali za kuwekeza katika sekta ya Maji, pia aliridhika na kazi zinazofanywa na DAWASCO pamoja na DAWASA za kuhakikisha wakazi wa Dar es salaam na Pwani wanapata huduma bora ya Majisafi hasa wale ambao bado maeneo yao hayajafikiwa na miundombinu ya huduma ya Majisafi.

"Tumeona kazi kubwa na nzuri inayofanywa na DAWASCO na DAWASA, tumejionea namna ambavyo serikali imewekeza katika sekta hii ya Maji, na namna ambavyo kazi kubwa ya kutibu, kusafisha na kusafirisha Maji inavyofanyika hadi hatua ya kumfikia mlaji, hakika sio kazi nyepesi, inahitaji nguvu na kujituma zaidi ili watu wote waweze kupata huduma bora” alisema Prof. Mbwete.

Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASCO, Mhandisi Cyprian Luhemeja, alisema kuwa ziara ya bodi ya DAWASCO imekuja wakati muwafaka ambapo Shirika hilo lipo katika kupambana pamoja na kumaliza tatizo la upotevu wa Maji katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam na Mkoa wa Pwani.

Aidha, ameeleza kuwa maeneo mengi ambayo yalikuwa na changamoto ya huduma ya Majisafi kwa sasa yanapata huduma hiyo, hasa katika maeneo ambayo yapo pembezoni mwa barabara ya Morogoro kuanzia Mbezi, Kimara, Ubungo pamoja na maeneo mengi ya Tabata kwa sasa wanapata huduma ya Majisafi, hasa baada ya kukamilika kwa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu.

“Mitambo hii ya Ruvu juu na Chini ina hudumia sehemu kubwa ya Jiji la Dar es salaam pamoja na Mkoa wa Pwani, hivyo kutokana na upanuzi uliofanyika katika mitambo hii maeneo mengi sasa yanapata huduma Majisafi ya kutosha na hata yale maeneo yaliyokuwa na changamoto kutokana na miinuko, sasa yanapata huduma”. alisema Mhandisi Luhemeja.

Bodi ya DAWASCO iliyozinduliwa mapema na Mh Waziri wa Maji ,Mh Isack Kamwele mapema wiki hii imekuwa ni bodi ya Tano tangu shirika hilo kuanza majukumu yake ya kuzalisha na kusambaza Maji katika Mkoa wa Dar es salaam pamoja na miji ya Kibaha na Bagamoyo mkoani pwani ambapo itakuwa chini ya Mwenyekiti wake Profesa Tolly Mbwete.
Na Hellen Kwavava - Dar es salaam
Theme images by rion819. Powered by Blogger.