ATUPWA JELA MIAKA 10 KWA KUKUTWA NA BASTOLA,RISASI


MFANYABIASHARA Gairo Mtozoma (43) amehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kukutwa na hatia ya mashitaka mawili ya kupatikana na silaha na risasi.

Mtozoma ambaye pia ni mkazi wa Magomeni Kagera, alihukumiwa kifungo hicho jana mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa.

Hakimu Mwambapa alisema kuwa upande wa mashitaka, ulikuwa na mashahidi watano kwa ajili ya kuthibitisha mashitaka hayo na kwamba baada ya kusikiliza ushahidi huo, mahakama ilimuona mshitakiwa kuwa na kesi ya kujibu na kujitetea mwenyewe.

Alisema katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi, mashitaka ya kwanza ya kupatikana na silaha, mshitakiwa huyo atatakiwa kutumikia kifungo cha miaka mitano jela na katika mashitaka ya pili atatumikia kifungo cha miaka mitano. 

Kabla ya kutolewa kwa adhabu, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa iwe fundisho kwa wengine.

Katika kesi ya msingi, inadaiwa Agosti 11, mwaka jana maeneo ya Magomeni Kagera wilayani Kinondoni, Mtozoma alikutwa na bastola moja aina ya Browing yenye kumbukumbu namba 90002 iliyosajiliwa kwa namba TZCAR-A222683 bila kuwa na leseni.

Pia inadaiwa Agosti 11, mwaka jana maeneo ya Magomeni Kagera wilayani Kinondoni alikutwa na risasi sita bila kuwa na leseni.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527