MAZOMBI WA SIMU KUPIGWA FAINI WAKIVUKA BARABARANI

Honolulu limekuwa jiji la kwanza kubwa nchini Marekani kuifanya kuwa haramu kwa "mazombi wa simu" kuvuka barabara wakitumia au kutazama simu zao.

Serikali katika jiji hilo la Hawaii wameidhinisha sheria ya kutotekwa fikira ukitumia kivuko cha barabarani.

Hii ina maana kwamba ni marufuku hata kuitupia jicho skrini ya simu yako kwa muda mfupi ukivuka barabara.

Ukipatikana na kosa hilo utapigwa faini ya $15-$35 (£11-£27).

Ukirudia kosa hilo, unaweza kutozwa faini ya hadi $99 (£76), shirika la habari la KHNL Hawaii News Now limeripoti.

"Ni jambo la kimsingi, kwamba macho yako huwa hayatazami pale unapotakiwa kutazama na hilo huweka kila mtu hatarini. Kutazama chini kidogo hata muda mfupi kuangalia ujumbe kwenye simu, unaweza kukosa kuangalia barabara kwa sekunde tano," afisa wa polisi wa Honolulu James Shyer ameambia KHNL.

Wanaotembea kwa miguu hata hivyo bado wataweza kutumia simu zao wakitembea maeneo yaliyotengewa abiria barabarani.

Aidha, unaweza kusamehewa iwapo utatazama simu yako kupiga simu ya dharura, shirika la habari la NPR limesema.

Sheria hiyo iliidhinishwa kuwa sheria Julai lakini kulikuwa na miezi mitatu ya kuwahamasisha raia kabla ya kuanza kutekelezwa rasmi.

Wakati huo, meya Kirk Caldwell alisema Honolulu ni mji ambao ulikuwa na sifa mbaya ya watu wengi kugongwa na magari kwenye vivuko vya barabara - hasa watu wazima - kuliko mji wowote ule Marekani.

Miji mingine imekuwa pia ikifikiria kuchukua hatua sawa.Kupiga simu ukivuka barabara bado ni haramu

Baraza la jiji la Toronto lilipiga kura kuomba serikali ya jimbo la Ontario kufanyia marekebisho sheria za trafiki kulifanya kuwa kosa mtu akitembea akiwa hisia zake zimetekwa.

Lakini serikali ya jimbo iliamua zaidi kuangazia kuhamasisha raia kuhusu hatari ya kufanya hivyo.

Afisa wa polisi wa Toronto Clint Stibbe aliambia CBC mnamo 25 Oktoba kwamba badala ya kupitisha sheria, abiria wanafaa kuwajibikia zaidi usalama wao.

Chanzo-BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post