Makubwa Haya : WANAWAKE WA KENYA WAGOMA KUFANYA MAPENZI MPAKA UHURU KENYATTA AWE RAIS

Jubilee wameiga kaulimbiu ya kampeni ya muungano wa Nasa baada ya kikundi cha wanawake kutoa wito wa kujizuia kufanya ngono hadi pale watakapokamilisha kumsimika Uhuru Kenya kuwa rais.


“Hakuna ngono hadi baada ya uchaguzi” ni kauli ya hamasa iliyoanzishwa na mgombea urais kwa tiketi ya Nasa, Raila Odinga kwamba wakati wa vita wanaume huwa hawalali na wake zao. Kauli hiyo ilikuwa maarufu kipindi cha kuelekea uchaguzi wa Agosti 8.


“Agosti 8 inakuja; itakuwa siku ya kihistoria na hakuna mtu atakayeachwa bila kupiga kura. Wanaume watalala nje. Siku itakapofika, hakuna mwanamume kulala na mkewe,” alikuwa akisema.


“Mnapokwenda vitani, ngono ni mkosi,” Odinga alinukuriwa akisema Juni.


Safari hii kikundi cha wanawake nchini kimetoa rai ngono ipigwe marufuku kuelekea uchaguzi mkuu wa marudio ambao umeamriwa na Mahakama ya Juu.


Ingawa sintofahamu imetawala uchaguzi huo uliopangwa Oktoba 26, wanawake katika mji wa Nyeri katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano walisema hawatashiriki ngono na waume zao hadi Uhuru Kenyatta atakapoapishwa kuwa rais kwa muhula wa pili.


Kiongozi wa kikundi hicho, Rahab Mukami, ambaye ni mwakilishi wa wanawake alisema wanawake wameimarisha kampeni kuhakikisha Kenyatta anashinda.


Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imesisitiza kwamba uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa licha ya mgomo ulioitishwa na Odinga wa National Super Alliance (Nasa).


Nasa wametoa wito kwa wafuasi wao kufanya maandamano makubwa siku ya uchaguzi. Mara kadhaa wafuasi wao wamepambana na polisi katika mitaa ambayo muungano huo ni ngome zao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527