TATIZO LA NGUVU ZA KIUME LATUA BUNGENI,MBUNGE AHOJI SERIKALI NAMNA YA KULIKABILI

Sakata la upungufu wa nguvu za kiume ambalo limekuwa changamoto kubwa kwa baadhi ya wanaume miaka ya sasa, limeibua sintofahamu bungeni baada ya mbunge wa Konde, Khatibu Saidi Haji (CUF) kutaka kujua serikali imejipanga vipi katika kukabiliana nalo.


Akijibu swali hilo Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamisi Kigwangala amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema  serikali haina jibu la moja kwa moja kuweza kuwapa wananchi, kwani tendo la ndoa hufanyika faragha baina ya wanandoa.

Dkt. Kigwangala aliendelea kusema kwamba pamoja na usiri uliopo kuhusu tatizo hilo, lakini kuna vitu wanaweza kufanya ili kukabiliana nalo, ambapo huweza  likasaidia kuokoa ndoa yao na kuweza kuwapatia watoto.

"Nianze kukubaliana na Mhe. Hatibu Said Haji kwa swali la msingi, changamoto za ukosefu wa nguvu za kiume zinazowapata wanaume wengi sasa hivi, zinatokana na ukosefu wa furaha, msongamano wa mawazo na ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, ukiwa na matatizo haya huwezi kuwa na furaha katika tendo la ndoa", alisema Dkt. Kigwangala.

Naibu huyo wa Wizara inayohusika na masuala ya Afya aliendelea kwa kuwataka wananchi watafute furaha binafsi ili kuweza kuwa na hamasa ya kufanya jambo hilo, na kuacha kuamini kwenye dawa za asili ambazo zimekuwa zikiuzwa kiholela bila kuzingatia usalama wake kwa afya ya mtumiaji

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post