Kamanda wa Polisi Kanda Maalum jijini Dar es salaam Lazaro Mambosasa, amesema watu waliokamatwa na polisi hapo jana kwa kufanya mkusanyiko usio rasmi, walishaonywa kutofanya hivyo lakini hawakujali hivyo sheria itachukua mkondo wake dhidi yao.
Kamanda Mambosasa amesema hayo leo na kusema kitendo cha kufanya mkusanyiko usio rasmi ni kuvunja sheria, hivyo lazima watafikishwa Mahakamani kujibu shtaka lao, huku akikanusha kuwakamata watu hao kwa kutokana na kuvaa t-shirt zilizoandikwa 'pray for Tundu Lissu'.
"Kwanza ifahamike hatujawakamata kwa kosa la kuvaa tshirt, zile ni nguo kama nguo nyingine wanavyovaa mashabiki wa Simba na Yanga, hawa walichofanya mpaka wakamatwe ni kufanya mkusanyiko usio rasmi na kibaya zaidi tulishawaeleza, na wenyewe walipoona polisi wanakuja wakaanza kutukimbia kwamba walijua wamefanya nini", amesema Kamanda Mambosasa.
Kamanda Mambosasa ameendelea kwa kusema jeshi la polisi linaendelea kuwahoji watu hao na kisha kupelekwa Mahakamani kusomewa mashtaka yao ili sheria ifanye kazi yake.