Picha: RC SHIGELA AFUNGUA MKUTANO MKUU WA UMOJA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA -UTPC MKOANI TANGAMkuu wa mkoa wa Tanga Martin Shigela leo Ijumaa Septemba 15,2017 amefungua mkutano Mkuu wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (Union of Tanzania Press Clubs- UTPC) mwaka 2017. 

Mkutano huo uliokutanisha viongozi wa Klabu za Waandishi wa Habari kutoka mikoa 27 nchini unafanyika katika ukumbi wa Tanga Beach Resort mkoani Tanga. 

Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo ambao utafanyika kwa muda wa siku mbili (Septemba 15 na 16,2017),Shigela alisema serikali inatambua umuhimu wa vyombo vya habari katika maendeleo ya jamii. 

“Ukitaka maendeleo katika jamii lazima ushirikiane na vyombo vya habari,na hata tunapoelekea katika Tanzania ya viwanda ni vyema vyombo vya habari vihusike”,alieleza. 

Alitumia fursa hiyo kuwataka waandishi wa habari nchini kuzingatia maadili katika kazi yao ya uandishi wa habari huku akiwaasa kujiendeleza kielimu ili kufanya vizuri zaidi katika kazi yao. 

“Vyombo vya habari vinafundisha,vinaelimisha,vinahamasisha ,vinakosoa na kufichua maovu na ili kutimiza haya ni vyema mkazingatia maadili yenu,mfanye kazi kwa usawa bila upendeleo lakini pia ni vyema mkawa wazalendo”,aliongeza. 

Kwa Upande wake rais wa UTPC,Deogratius Nsokolo alisema miongoni mwa changamoto zinazoikabili tasnia ya habari ni uwepo wa sera na sheria zinazobinya uhuru wa vyombo vya habari ikiwemo sheria ya Habari ya habari ambayo baadhi ya vifungu vyake siyo rafiki kwa waandishi wa habari. 

“Tunaiomba serikali ifanye marekebisho katika baadhi ya vifungu kwenye sheria hii ambavyo siyo rafiki kwa vyombo vya habari”,aliongeza Nsokolo. 

Awali akizungumza katika mkutano huo,Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC,Abubakar Karsan alisema mkutano huo umekutanisha pamoja wadau mbalimbali wa habari nchini na viongozi wa klabu za waandishi wa habari kutoka mikoa 27 ya Tanzania bara na Zanzibar ukifadhiliwa na SIDA. 

Alisema katika mkutano huo wajumbe wanoshiriki watafanya majadiliano mbalimbali kuhusu masuala mbalimbali yanayowahusu waandishi wa habari.

Habari na Kadama Malunde- Malunde1 blog,Picha zote na Oscar Assenga- Tanga Raha Blog
Mkuu wa mkoa wa Tanga Martin Shigela akifungua mkutano mkuu wa UTPC
Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC,Abubakar Karsan akizungumza wakati wa mkutano huo
Mkuu wa wilaya ya Tanga Thobias Mwilakwa akizungumza ukumbini
Rais wa UTPC,Deogratius Nsokolo akitoa hotuba
Makamu wa Rais wa UTPC,Jane Mihanji akizungumza ukumbini

ENDELEA KUANGALIA MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA 
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post