Picha 5 : ASKOFU SANGU AIBUKIA KWENYE MTI WA AJABU 'UNAOPOTEZA WATU KIMIUJIZA' GAMBOSHI


Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu ameubariki mti maarufu uliopo katikati ya kijiji cha Gambosi 'Gamboshi' ,kata ya Gambosi wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu ambao unadaiwa kuwa watu huwa wanapotea katika mazingira ya kutatanisha wakipita karibu na mti huo.

Askofu Sangu alifika katika mti huo Septemba 20,2017 alipokuwa katika misa ya Kipaimara katika kanisa la Mtakatifu Petro Gamboshi lililopo katika kijiji hicho cha Gambosi ‘Gamboshi’.

Askofu Sangu aliubariki mti huo ili kuondoa ile dhana ya kwamba mti huo unapoteza watu kimiujiza na kwamba Gamboshi ni eneo salama kwani watu wake sasa wana hofu ya mungu. 

Tukio hilo lilihudhuriwa pia na wazee wa kimila na waganga wa kienyeji,madiwani na wananchi wa eneo hilo.

Askofu Sangu alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa serikali kuyafikia maeneo ambayo yalikuwa yamesahaulika ikiwemo Gamboshi na kuyapelekea miundombinu na kuwafungua watu hao ili waweze kubadilika kifikra, kimaono na kimtazamo. 

“Viongozi wa ngazi za serikali waje kuyafikia maeneo haya,wanafunzi wote waliohitimu darasa la saba waende wote sekondari hata kama hawajafaulu ili kuibadili jamii yao iweze kuondokana na ukatili wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa sababu wote wamezaliwa na kuumbwa kwa sura na mfano wa mungu’’,alisema Askofu Sangu. 

Askofu Sangu alisema ikiwezekana wanafunzi wote waliohitimu elimu ya msingi kijijini hapo wawe wamefaulu au hawajafaulu waende shule za sekondari ili baada ya kuhitimu waweze kuibadilisha jamii ya eneo hilo baada ya kupata elimu. 

Askofu Sangu aliwaimarisha wakristo wapya zaidi ya 200 katika kanisa la Mtakatifu Petro Gamboshi lililofunguliwa na askofu huyo miezi michache iliyopita. 

Paroko wa parokia ya Ngulyati inayojumuisha eneo la Gamboshi John Nkinga alisema tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo hadi sasa kuna mabadiliko makubwa kutokana na watu wa eneo hilo wameanza kubadilika kiimani kwa kumcha Mungu. 

Gamboshi ni kijiji kinachosifika kuwa ndiyo makao makuu ya wachawi na tangu nchi ipate uhuru hakuna kiongozi mkubwa wa serikali amewahi kufika katika kijiji hicho,lakini kwa namna ya pekee Askofu huyo mara tu baada ya kuteuliwa kuwa askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga,aliamua kukifia kijiji hicho kisha kuanzisha kanisa. 
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu akibariki mti unaodaiwa kupoteza watu katika mazingira ya kutatanisha uliopo katikati ya kijiji cha Gamboshi-Picha zote na Isack Edward Kisesa - Malunde1 blog
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu akibariki mti huo
Wananchi wakiwa katika mti huo
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu akiwa katika mti huo
Muonekano wa mti huo kwa mbali.

Picha zote na Isack Edward Kisesa - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527