MCHUNGAJI MSIGWA ATAJA ORODHA YA WABUNGE WA CHADEMA ALIODAI WAPO KWENYE ORODHA YA KUUAWA


Mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya CHADEMA Peter Msigwa amefunguka na kutaja majina ya wabunge wengine wa nne ndani ya CHADEMA ambao wamekuwa wakiwindwa na watu wasiojulikana ili kushambuliwa kama alivyoshambuliwa Mbunge Tundu Lissu.


Msigwa amesema hayo leo akiwa jijini Nairobi nchini Kenya ambapo yupo huko kwa ajili ya kumuangalia Mbunge Tundu Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi Septemba 7 mwaka huu mjini Dodoma


Msigwa ametumia nafasi hiyo kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama kuwa hata wao wanatafutwa na watu wasiojulikana ili kupigwa risasi.


"Usalama wetu upo mashakani niwaambie usalama wa taifa, nimwabie Mkuu wa Majeshi, nimwabie IGP pamoja na Rais mwenyewe tunawindwa wabunge wengine wanne wa CHADEMA akiwepo Mhe. Freeman Mbowe, mimi vijana wale walinifuata wiki mbili zilizopita Iringa, Mhe Godbless Lema alifuatwa Arusha, Halima Mdee na Mhe. Mbowe tupo kwenye orodha hiyo ya kuuwawa" alisema Mchungaji Msigwa


Aidha Mchungaji Msigwa ameendelea kusema licha ya vitisho hivyo wao wataendelea kuzungumza na kukemea mambo ambayo yapo kinyume na utaratibu na sheria za nchi na kusema hawataogopa.


"kwa hiyo hizo roho zetu tumeziweka mikononi mwenu lakini tunasema kwamba hatutanyamaza tutakosoa, tukakemea, na kupinga uonevu wowote katika nchi yetu, kwa haya mambo hamtatutisha wala kutunyamazisha tunaendelea kusonga mbele" alisema Mchungaji Msigwa.
Via>>Mpekuzi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post