JWTZ YATIMIZA MIAKA 53 TANGU KUANZISHWA KWAKE

Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) leo (jana) limetimiza miaka 53 tangu kuanzishwa kwake ambapo akiongeza na waandishi wa habari Jenerali mabeyo aliwaambia waandishi kuwa yuko na Jenerali Sarakikya (rtd) Mkuu wetu wa Majeshi ya Ulinzi wa Kwanza Mzalendo, Jenerali Mwamunyange (rtd) Mkuu wa Majeshi wa Saba, ambaye nimepokea kijiti hiki toka kwake mwezi Februari, 2017.


Wapo pia, Mnadhimu Mkuu wa Jeshi Luteni Jenerali Mwakibolwa, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Isamuhyo, Wakuu wa Kamandi, Wakuu wa Matawi (Machifu) wa Makao Makuu ya Jeshi na Sajini Meja wa Jeshi letu.


Nimeona nijumuike nao wote hawa ili kwa pamoja kupitia kwenu Waandishi wa Habari mtuwasilishie salamu zetu za Maadhimisho ya Miaka 53 ya JWTZ, kwa Watanzania wote. Maadhimisho haya yalianza tarehe 25 Agosti, 2017 kwa Wanajeshi wote kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo Michezo, kufanya Usafi kwenye maeneo ya kijamii na Tiba. Leo hii tunahitimisha Madhimisho hayo.


Siku hii ya leo JWTZ linasherehekea kutimiza miaka 53 tangu kuundwa kwake Septemba Mosi, 1964. Hii ni siku muhimu sana kwetu na kwa wananchi wa Tanzania kwa ujumla, kwa sababu, JWTZ ni Jeshi letu sote na limeundwa kutokana na Wananchi wa Tanzania. Awali ya yote kwa heshima na taadhima ninapenda kutumia fursa hii kumshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniamini na kuniteua kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi. Pili kwa niaba ya JWTZ na kwa niaba yangu mwenyewe napenda kumshukuru Waziri wa Ulinzi na JKT, pamoja na Wizara anayoiongoza kwa mwongozo anaotupatia na ushirikiano mkubwa anaoutoa kwa Jeshi.


Aidha, Wakati tunatimiza Miaka 53 napenda pia kuwashukuru Baraza la Mawaziri pamoja na Viongozi Wakuu wa Serikali kwa Maelekezo mbalimbali wanayoyatoa kwa Jeshi letu. Ushauri wao umekuwa mhimili mkubwa kwa utendaji wa Jeshi letu. Ninawashukuru pia Wakuu wa Majeshi Wastaafu, wengine ninao hapa leo mnawaona kwa namna walivyolilea Jeshi letu katika nyakati mbalimbali hadi hii leo tunatimiza miaka 53 likiwa Jeshi kubwa kabisa, lenye nidhamu kubwa, weledi na uhodari mkubwa.


Wakati tunaandika Historia ndefu ya Miaka 53, Jeshi letu limefikia mafanikio mbalimbali, miongoni mwa mafanikio ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) ni kudumisha amani na utulivu uliopo nchini mwetu tangu Taifa letu lipate Uhuru wake. Aidha, JWTZ limeshiriki Vita vya ukombozi Kusini mwa Afrika, Vita vya Kagera na Visiwa vya Comoros. Jeshi letu pia limekuwa ni nguzo muhimu katika kudumisha amani sehemu mbalimbali duniani kwa kushiriki katika shughuli za Ulinzi wa Amani, katika nchi za Liberia, DRC, Sudan (Darfur), Lebanon, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati n.k. Ndani ya Nchi Jeshi letu limeshiriki kutoa usaidizi katika masuala mbalimbali ikiwemo majanga, uokoaji na huduma za kijamii. JWTZ bado limeendeleza mshikamano na kuonesha uzalendo wa hali ya juu na hivyo kubakia kuwa Jeshi la Wananchi.


Naomba niwatakie Maafisa na Askari wa JWTZ na Watanzania kwa ujumla “Happy Birthday”. Ninawapongeza sana kwa kufikia siku ya leo. Kwa vile leo ni siku ya Eid El Hajj nawatakia Eid Njema pia wao na familia zao.


Mwisho, ninawaomba watanzania wote waliunge mkono Jeshi lao na JWTZ daima liko imara na tayari kuilinda Nchi yetu. Tutailinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuitumikia kwa uaminifu Serikali yetu. Namuomba Mungu atusaidie.


JENERALI VENANCE SALVATORY MABEYO, ndc


MKUU WA MAJESHI YA ULINZI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post