WASOMI WAHOJI UZALENDO WA TUNDU LISSU


BAADHI ya wasomi nchini wamehoji uzalendo wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu wa kushabikia matatizo ya nchi yake badala ya kuwa sehemu ya kutafuta ufumbuzi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Profesa Benson Bana ameelezea kitendo cha Lissu kujitokeza mbele kwa mbwembwe suala la kuzuiliwa kwa ndege ya Tanzania nchini Canada, ni kitendo kinachozua maswali mengi juu ya uzalendo wake kwa Tanzania.

“Nilipomuona amejitokeza katika vyombo vya habari ilinishtua kwa sababu tangu mwanzo Lissu na wenzake walikuwa wanapinga ujio wa hata zile ndege mbili za mwanzo,” alieleza Profesa Bana.

 Alieleza kuwa mwenendo ambao Lissu ameendelea kuuonesha, unaashiria kuna walakini mkubwa katika suala la uzalendo na pia kujenga hisia kwamba inawezekana kuna jambo nyuma ya pazia, linalomsukuma kufanya mambo yanayoharibu maslahi ya Taifa.

Msomi huyo alisema hivi sasa kumekuwa na minong’ono mingi juu ya uzalendo wa Lissu na namna anavyosemekana kushirikiana na watu wa nje katika kuiumiza nchi. 

“Tuliosoma somo la Uraia tulifundishwa namna ya kuipenda nchi yako na kutumia uwezo wako kuisaidia nchi yako badala ya kuivua nguo,” alisitiza Profesa Bana huku akimfananisha mwanasiasa huyo na askari aliyoko vitani, anayeuza siri za jeshi badala ya kupambana kulisaidia jeshi lake kushinda vita.

Aidha, alieleza pia kutokufurahishwa na kitendo cha Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACTWazalendo) cha kumuuliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kupitia akaunti ya tweeter kuhusu kutokuwasili kwa ndege ya Bombardier Q400-Dash 8, ambapo Profesa Bana ameielezea njia hiyo ya mawasiliano kama si sahihi na badala yake angeweza njia ambayo si ya kila mtu kujua.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Wakili Dk Damas Ndumbaro amemuelezea Lissu kama mtu anayetafuta umaarufu kwa njia yoyote ile hata kama njia anayoitumia itakuwa na madhara kwa maslahi ya nchi.

“Haya tunayoyaona kwa Lissu inatuonesha jinsi gani upeo wake upo kiuanaharakati zaidi kuliko uongozi na katika hili ni kama bomu linalosubiri kulipuka ambalo hata viongozi wa chama chake na hata wafuasi wake wanashindwa kuling’amua,” alieleza Dk Ndumbaro. Maneno ya Dk Ndumbaro yaliungwa mkono ya Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja ambaye alisema tatizo kubwa la Lissu ni kukosa maarifa ya uongozi.

“Lissu hajui uongozi na hii ndiyo shida kubwa inayomkabili. Hajui suala la maslahi ya nchi katika siku zijazo na siku zote amekuwa akiona mabaya,” alieleza Profesa Semboja. Kwa upande wake, mtaalamu wa sheria za kodi ya madini, Dk Hellen Kihunsi alisema hata kama kuzuiwa kwa ndege ni suala la kisheria lakini Tundu Lissu alipaswa kutumia njia bora zaidi ya kuwasilisha kwa mamlaka husika badala ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari.

“Masuala kama haya yana maslahi kwa Taifa mbapo hata yeye (Lissu) ni sehemu ya Taifa hili, lakini kwa mwenendo ambao siku zote amekuwa akiuonesha unatilia shaka uadilifu na uzalendo wake kwa Taifa,” alieleza Dk Kihunsi. Tangu Serikali ya Awamu ya Tano ianze kuchukua juhudi ya kuifufua Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), kumekuwa na baadhi ya wanasiasa kutoka vyama vya upinzani wakipinga juhudi hizo, ambapo ndege mbili za awali aina ya Bombardier zilipigiwa kelele na wapinzani wakidai hazifai licha ya kwamba zimekuwa msaada mkubwa katika sekta ya usafirishaji.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post