SUMAYE : SIPO TAYARI KURUDI CCM KWA KUTESWA

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye amefunguka na kusema licha ya mambo anayofanyiwa na serikali ikiwa pamoja na kunyang'anywa mashamba yake lakini hawezi kurudi CCM.

Sumaye amedai kuwa toka alipohama chama hicho na kuingia upinzani wapo viongozi walitamka wazi kuwa dawa yake ni kupokonywa mali zake mpaka awe masikini na kudai hayo mambo ndiyo yameanza lakini hayawezi kumfanya kurudi tena katioka chama hicho.

"Hata lile lililotokea Mwabepande nililitegemea kama mtakumbuka kipindi nilichohama kutoka CCM na kuja upinzani mwaka 2015 katika kipindi cha kampeni wapo viongozi walitamka wazi kuwa huyu dawa yake kunyang'anywa mali zake mpaka awe masikini, nilipoanza kuandikiwa barua mara sijafanya hiki sijui sijafanya hiki nikajua wazi kuwa hakuna sababu nyingine zaidi ya sababu za kisiasa na nina adhibiwa kwa kuwa nimekwenda upinzani" alisema Sumaye.

Aidha Sumaye amekiri kuwa mashamba hayo aliyapata kwa njia halali na siku zote amekuwa akiyalipia kwa muda wote huo na kusema mashamba yake yeye amekuwa akiyaendeleza tofauti na inavyoelezwa kuwa mashamba hayo hayaendelezwi.

"Mimi nitaiachia mahakama iendelee mpaka hapo itakaposema ama imeshindwa ama nifanye nini kama wanafikiria mimi nitarudi CCM kwa kuteswa, nasema sirudi CCM eti kwa sababu nateseka" alisisitiza Sumaye

Serikali imetangaza kuchukua mashamba mbalimbali ya wananchi ambayo hayajaendelezwa kwa muda mrefu na wamiliki wa waeneo hayo, jambo ambalo limemkuta na Mhe. Sumaye kwa mashamba yake mawili kudaiwa kuchukuliwa na serikali kwa kigezo hicho hicho kuwa hayajaendelezwa kwa muda mrefu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post