RUGEMALIRA WA ESCROW ANYIMWA DHAMANA MAHAKAMA YA MAFISADI

Mshtakiwa wa kesi ya uchotaji fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, James Rugemalira amegonga ukuta katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi (Mahakama ya Mafisadi) baada ya kunyimwa dhamana.

Rugemalira ambaye anakabiliwa na kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, yenye mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana, alikimbilia mahakamani hapo kuomba afutiwe mashtaka ya utakatishaji fedha kisha aachiwe huru kwa dhamana kwa madai hati ya mashtaka yanayowakabili ina kasoro za kisheria.


Jana, Jaji Mfawidhi Firmin Matogolo alitupilia mbali maombi hayo akisema Mahakama hiyo haina mamlaka ya kumpa nafuu alizokuwa akiziomba.


Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, jopo la mawakili wa Rugemalira waliieleza Mahakama kuwa hati ya mashtaka haina maelezo yanayoonyesha kosa la utakatishaji fedha.


Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Dk Zainabu Mango alipinga hoja hizo, akidai mashtaka yanayomkabili mshtakiwa hayana dhamana.


Akijibu hoja ya kasoro za hati ya mashtaka, Wakili Mango alidai maombi hayo yamepelekwa kwenye jukwaa ambalo si sahihi.


Alisema kesi hiyo haijafikia hatua ya kusikilizwa katika mahakamani hiyo na kwamba inaweza kuangalia uhalali wa mashtaka hayo, shauri hilo litakapohamishiwa mahakamani hapo kwa usikilizwaji.


Hata hivyo, Jaji alikubaliana na hoja za Wakili Mango kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kuchunguza uhalali wa hati ya mashtaka kwa kuwa suala hilo limefikishwa wakati ambao si muafaka.


Pia, Jaji Matogolo alisema kwamba Mahakama hiyo huwa na mamlaka ya kuchunguza uhalali wa mashtaka endapo maombi yangewasilishwa kwa njia ya mapitio na si dhamana.


Rugemalira na mshirika wake wa Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Harbinder Singh Sethi wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527