RUBANI AFARIKI DUNIA BAADA YA NDEGE YAKE KUANGUKA ARUSHA

RUBANI wa ndege ndogo, mkazi wa Dar es Salaam, David Mbale (25), amefariki dunia baada ya ndege aliyokuwa akiendesha kuanguka kwenye vilima vya Monduli mkoani Arusha.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema tukio hilo lilitokea juzi katika Kijiji cha Engalaoni kilichopo mpakani mwa wilaya za Monduli na Arumeru.


Kwa mujibu wa Kamanda Mkumbo, Mbale alikuwa akiendesha ndege ndogo yenye namba za usajili 5HSAL 206 inayomilikiwa na Kampuni ya Safari Air Link.

“Ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria watano, iliondoka katika uwanja mdogo wa ndege wa Arusha, majira ya saa 1:30 asubuhi ya siku hiyo ya tukio ikielekea katika eneo la Kogatende, Serengeti kuwachukua watalii.

“Kwenye ndege hiyo, alikuwamo rubani peke yake na alikuwa anasubiriwa na watalii huko Serengeti.

“Taarifa za kuanguka kwa ndege hiyo zilianza kuenea juzi saa nne asubuhi, zikisema kuna ndege imeanguka katika vilima vya Monduli ambavyo ni maarufu kama Monduli Hills.

“Baada ya taarifa hizo kutolewa saa 6:30, tuliwajulisha kikosi cha zimamoto na wenzetu wa uwanja wa ndege wa Arusha na walipofika kwenye kilima hicho, walikuta rubani ameshafariki dunia na mwili wake ulichukuliwa kwa uchunguzi zaidi,” alisema Kamanda Mkumbo.

Wakati huo huo, Kamanda Mkumbo alisema uchunguzi wa tukio hilo umeanza jana na kwamba watashirikisha wataalamu waliobobea katika masuala ya ndege.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527