Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohammed Janab ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo August 30, 2017 kuwa moyo wa Mfanyabiashara Yusuf Manji umewekwa vyuma ili kumsaidia kupumua.
Prof. Janab ambaye ni Daktari wa moyo na Shahidi wa kwanza upande wa utetezi ameyasema hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha wakati akitoa ushahidi katika kesi ya dawa za kulevya inayomkabili Manji ambapo akiongozwa na Wakili wa utetezi, Hajra Mungula, alisema yeye ni Daktari wa moyo wa Taasisi ya JKCI.
Amesema anamfahamu Manji baada ya kufikishwa katika Taasisi hiyo February 2017 akiwa mwenye matatizo ya moyo na kuongeza kuwa alipofikishwa hapo alifanyiwa vipimo na jopo la madaktari lililobaini Moyo wake umewekewa vyuma ambapo akaingizwa mipira maalum na kubaini kwamba upo katika hali nzuri.
”July 2017 alirudishwa tena katika Taasisi yetu akiwa na tatizo hilo la moyo pamoja na maumivu ya mgongo na kutokuwa na usingizi.”
Prof. Janab amesema alivyorudi hapo walimpokea kama mgonjwa aliyetibiwa nje ya nchi na ripoti ilionyesha ametibiwa Florida, Marekani.
Alipoulizwa na Wakili Mungula kama mgonjwa aliyewekewa vyuma katika moyo anaweza kutumia dawa za kulevya, Prof. Janab alijibu kwamba huwa haruhusiwi kufanya baadhi ya mambo ikiwemo kuvuta sigara, kutumia Heroin
Prof. Janab ameongeza kuwa katika awamu ya pili ya Manji kurudi hospitalini hapo walimsaidia kumtibia maumivu aliyokuwa nayo kwa kumpa Drip ya Paracetamol’s na Sindano ya Tram a do.
Akijibu hoja ya Wakili wa Serikali, Timony Vitalis kwamba matumizi ya dawa za kulevya yanaweza kusababisha ugonjwa wa moyo, Prof. Janab alijibu ndio.
Kesi imeahirishwa hadi August 31, 2017 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.