STAND UNITED 'CHAMA LA WANA' YAPATA UDHAMINI WA MILIONI 100 KUTOKA KAMPUNI YA BIKO


Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mheshimiwa Stephen Masele akizungumza katika mkutano wa hadhara leo Mjini Shinyanga-Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog

*****

Wakati pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2017-2018 likitarajiwa kufunguliwa rasmi kesho Agosti 27, mwaka huu kwa timu zote 16 kuingia viwanjani,Kampuni ya Michezo ya Bahati Nasibu Mtandaoni – BIKO imeidhamini Klabu ya Stand United ‘Chama la Wana’ shilingi milioni 100 kuanzia mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Ijumaa,Agosti 25,2017mjini Shinyanga, Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mheshimiwa Stephen Masele (CCM) alisema BIKO wameamua kuidhamini timu hiyo baada ya kuridhishwa na mwenendo wa timu hiyo. 

“Baada ya Stand United kupoteza mwelekeo na wadhamini wake Kampuni ya Acacia kujiondoa katika udhamini,hivi sasa nimeamua kuwa msimamizi mkuu wa timu hii,nimetafuta udhamini mwingine,nimeiomba kampuni ya Kitanzania ya BIKO,imekubali kuwa wadhamini wakuu na imetupatia shilingi milioni 100 kwa mwaka huu”,alieleza Masele. 

Mbunge huyo alisema ameamua kuwa msimamizi mkuu wa timu hiyo ili kuhakikisha kuwa timu hiyo inafanya vyema katika michezo mbalimbali.

“Najua mnaelewa uhusika wangu katika Stand United,mnafahamu jitihada nilizofanya kuhakikisha timu hii inafanya vizuri,ili timu hii iwe ya kimataifa na timu hii baada ya kupata matatizo yaliyotokea,ilikuwa kama timu yatima,haina ulezi,haina msaada,na mimi kama mbunge nilikuwa nimekasirika na nikasema Maeja na wenzake wasinisumbue katika mambo ya mpira”,alisema. 

“Nilitafuta ufadhili wa shilingi bilioni 2.4 kutoka Acacia,lakini tuliuchezea,na baada ya kujiridhisha na uongozi mpya ulioingia ukiongozwa na Dk. Maeja nimetafuta wadhamini wengine ambao ni kampuni ya BIKO ili kuisadia timu yetu,naomba fedha hizi zitumike vizuri”,alisema Masele. 

Masele alitumia fursa hiyo kuwatahadharisha viongozi wa timu kuhusu matumizi mabaya na ubadhirifu wa fedha zilizotolewa na wadhamini hao na kuwa hawatasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.

“BIKO itapenda kuona fedha hizi zinatumikaje na kuanzia sasa mtu yeyote atakayejihusisha na ubadhirifu tutamfikisha katika vyombo vya sheria kwa sababu wanaumiza hisia za watu wengi”,aliongeza Masele. 

“Nataka niwahikikishie kuwa timu hii haitashuka daraja kinatochotakiwa ni kutoa msaada kwa timu hii ikiwemo kuishangilia,jambo jingine naomba mjitahidi kubana matumizi katika masuala mbalimbali ikiwemo pale mnaposafiri punguzeni idadi ya watu wa kusafiri lakini pia lipeni mishahara ambayo haiumizi sana”,aliongeza.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Klabu ya Stand United,Dkt. Ellyson Maeja alisema Klabu hiyo ya Stand United imejipanga vizuri kuhakikisha kuwa inafanya vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2017-2018.

"Hivi sasa timu imetulia kiuongozi tatizo ni bajeti,mpira ni pesa,bila pesa hakuna timu,lakini pia hatuna usafiri wala hosteli kwa ajili ya wachezaji,tunaomba wadau waendelee kujitokeza kuisaidia timu hii,tumesajili wachezaji wapya 19,jumla sasa wapo 30,tunaye kocha mzuri,walimu wazuri,malengo yetu ni kushika nafasi ya kwanza hadi ya tatu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu wa 2017-2018",alisema Dkt.Maeja.


Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mheshimiwa Stephen Masele akizungumza katika mkutano wa hadhara leo Mjini Shinyanga ambapo alisema kampuni ya BIKO imedhamini timu ya Stand United kwa kuipatia shilingi milioni 100.

Wadau mbalimbali wakiwa katika mkutano huo.

Mwenyekiti wa Klabu ya Stand United,Dkt. Ellyson Maeja akielezea jinsi timu hiyo ilivyojipanga kufanya vizuri katika michezo mbalimbali huku akiomba wadau kuendelea kujitokeza kuisadia timu hiyo.
Dkt.Maeja akizungumzia masuala mbalimbali kuhusu Stand United.
Wananchi wakiwa katika mkutano huo.

Mheshimiwa Stephen Masele akisikiliza kwa makini maelezo kutoka kwa Dk. Maeja.

Diwani wa kata ya Kambarage katika manispaa ya Shinyanga,Hassan Mwendapolea akizungumza katika mkutano huo.

Wananchi wakiwa katika mkutano huo.
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post