MFANYABIASHARA AUAWA CHOONI AKIWA CLUB MJINI SINGIDA


Angel Edward enzi za uhai wake
Kamanda wa polisi mkoa wa Singida ACPDebora Magiligimba.
****

JESHI la Polisi mkoani Singida linawashikilia watu wawili kutokana na kifo cha mashaka cha mfanyabiashara, Tausi Hamisi au Angel Edward (39) mkazi wa eneo la Ipembe mjini Singida. 

Kamanda wa polisi mkoa wa Singida, Debora Magiligimba aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni Haruna Athuman (34) mlinzi wa Katala Beach Hotel (KBH) ambaye anaishi eneo la Kindai mjini Singida na Salma Mohamed (28) mkazi wa Majengo katika Manispaa ya Singida. 

Magiligimba alisema kuwa tukio hilo ni la Agosti 24, mwaka huu saa 11.30 alfajiri ambapo inadaiwa kuwa mwili wa mfanyabiashara huyo ulikutwa pembeni mwa choo cha wanawake katika hoteli hiyo. 

Alisema kuwa siku ya Jumatano Agosti 23, mwaka huu majira ya jioni marehemu aliondoka nyumbani kwao akiwa na gari yake ndogo kisha kuungana na wenzake kwenda ukumbi wa Taasisi ya Uhasibu (TIA) eneo la Ginnery mjini hapa ambapo kulikuwa na harusi. 


Hata hivyo, Magiligimba alidai kuwa baadae usiku huo marehemu akiwa na wenzake walienda Skyway Night Club eneo la Kibaoni alikokuwa anatumbuiza mwanamuziki mashuhuri, Christian Bella kuendelea na starehe. 

Inadaiwa baada ya muda, alitoka Skyway na kwenda KBH akiwa ameambatana na rafiki yake aitwaye Salma Mohamed pamoja na mwanaume mmoja ambaye hakufahamika jina wala makazi yake mara moja ambapo inasemekana waliendelea na starehe hotelini hapo. 

"Ilifika muda marehemu alienda kujisaidia chooni ndipo mwanaume huyo aliyekuwa amekaa naye alimfuata. Hakuweza kurejea tena hadi mlinzi alipogundua mwili wa marehemu alfajiri. Muuaji aliondoka na simu ya marehemu huku akiacha gari lake hotelini hapo", alisema. 

Kwa mujibu wa Kamanda Magiligimba, uchunguzi wa daktari unaonesha kuwa chanzo cha kifo cha marehemu ni kukosa hewa na kwamba hakuna dalili zozote za kunyongwa shingo.

Ametoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kubadilika na kuacha tabia ya kuambatana na watu wasiowafahamu kwenye maeneo ya starehe na inapotokea wawe wepesi wa kudadisi na ikiwa watamtilia shaka watoe taarifa polisi haraka.

Na Abby Nkungu- Malunde1 blog Singida

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527