WAZIRI MKUU AZISIFU TAASISI ZA AGHA KHAN.... ASISITIZA TANZANIA NI SALAMA KWA UWEKEZAJI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia uwekezaji wenye tija wawekezaji watakaokuja nchini kwa kuwa Tanzania ni nchi yenye amani,utulivu wa kisiasa na uchumi wenye kukua kwa kasi.

Ameyasema hayo jana Julai 09,2017 alipomuwakilisha Rais Dkt.John Magufuli katika maadhimisho ya miaka 60 tangu Mtukufu Aga Khan alipochaguliwa kuwa Imamu Mkuu wa madhehebu ya Shia Ismailia duniani.

Waziri Mkuu alisema Serikali inatambua na kuthamini shughuli mbalimbali zinazofanywa na mtandao wa taasisi za Aga Khan zilizopo hapa nchini, hivyo Serikali itaendelea kushirikiana nao.

Aliupongeza mtandao wa taasisi za Aga Khan kwa kumuunga mkono Rais Dkt.Magufuli katika kutoa kipaumbele cha kuwapa fursa watu wenye kipato cha chini kushiriki katika uzalishaji ili waweze kujikwamua kiuchumi.

"Nawahakikishia kwamba uwekezaji wenu hapa nchini utakuwa na baraka  kwa sababu nchi imetulia kisiasa na uchumi wake unakua kwa kasi. Nawaomba muendelee kuwaalika wanajumuia wa  madhehebu ya Shia Ismailia popote walipo duniani waje kuwekeza nchini fursa bado zipo", Majaliwa.

Kwa upande wake Rais wa Jumuiya ya Madhehebu ya Shia Ismailia Tanzania, Bw. Amin Lakhani aliishukuru Serikali kwa ushirikiano inaowapa na kwamba ameahidi kuendelea kushirikiana nayo katika kuboresha sekta mbalimbali nchini.

Alisema mtandao wa maendeleo wa Aga Khan unatoa huduma mbalimbali zikiwemo za afya,elimu,kilimo na kunaendesha miradi katika mabara ya Afrika na Asia kwa kuwapa fursa watu wenye kipato cha chini kushiriki katika uzalishaji ili kujikwamua kiuchumi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post