TREKTA LAPINDUKA NA KUUA ,WAWILI WAKAMATWA WAKIPELEKA GOBORE ZIFANYIWE MATAMBIKO SHINYANGA


NB-Siyo trekta lililoua

Mkazi wa kijiji cha Solwa kata ya Solwa wilaya ya Shinyanga Lucas Omethusela (46) amefariki dunia baada ya tela la trekta alilokuwa amepanda kupinduka.


Kwa mujibu wa taarifa ya kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro kwa vyombo vya habari,tukio hilo limetokea Julai 17,2017 saa 12 asubuhi katika kijiji hicho.

Alisema tela la trekta aina ya Massey Ferguson lenye namba za usajili T740 DJU likiendeshwa na dereva ambaye hajafahamika lilipinduka na kusababisha kifo cha mtu huyo huku Ndamo Cherehani (38) akipata majeraha.


Kamanda Muliro alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na kwamba ufuatiliaji wa kumtia mbaroni dereva husika.


Wakati huo huo Kamanda Muliro alisema wanamshikilia mtu mmoja aitwaye Obadia Munya (32) mkazi wa Mhongolo wilayani Kahama kwa kuuza pikipiki inayodhaniwa kuwa ni ya wizi.


Alisema askari wa kikosi cha upelelezi walimkamata mtu huyo akiuza pikipiki yenye namba za usajili T559 BEZ ,Engine SL157 FMI 16906998,Chassis namba LBRSPJB57G9004812 aina ya SUNLG huku akiwa na kadi ya kughushi akiuzia pikipiki hiyo.

Katika hatua nyingine alisema jeshi hilo pia limewakamata watu wawili wakazi wa Kaliua mkoa Tabora wakiwa na silaha tatu aina ya gobore zinazodaiwa kutumika katika vitendo vya uhalifu katika mkoa wa Shinyanga na mikoa ya jirani wakizipeleka kwa mganga wa kienyeji zikafanyiwe matambiko.

Kamanda Muliro alisema watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani haraka iwezekavyo upelelezi ukikamilika.
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post