RAIS MAGUFULI KUFUNGA MIGODI

RAIS wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli ametishia kufunga migodi yote inayomilikiwa na makampuni ya nje ikiwa makampuni hayo yatasshindwa kuanzisha mazungumzo haraka juu ya umiliki wao pamoja na tozo wanazopaswa kulipa.

Rais Magufuli ameyasema hay oleo katika mkutano wa hadhara katika wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma ambapo yupo kwa ziara ya siku tatu. Amesema haiwezekani makampuni hayo yanaendelea kuwa kimya wakati wameshakubaliana kuanzisha mazungumzo haraka.

"Makampuni ya madini yaliyoahidi kukaa na serikali kuzungumza, wafanye haraka wakiendelea kuchelewa nitafunga migodi yote wanayomiliki" Rais Dk John Pombe Magufuli, leo Kakonko, Kigoma.

Katika Mkutano huo Rais Magufuli amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla kuwa ataendelea kupambana na kodi zenye kuwakera wananchi hasa wananchi wa hali ya chini.

Amesema mpaka sasa serikali imeondoa kodi katika kilimo na mazao takribani 80 ambazo zilikuwa kero kwa wakulima na itaendelea kuzipunguza mpaka wakulima wafaidike na kilimo hicho.

“Tumefuta tozo 80 katika kilimo na mazao. Tushikamane wakulima wote ili kuendeleza nchi yetu, na tumefuta tozo zaidi ya 50 katika mifugo na bado tutaendelea kuzifuta tozo kwa wananchi wanyonge ili wafaidike na kilimo pamoja na ufugaji” amesema Rais Magufuli.

Kwa muda mrefu wakulima vijijini wamekuwa wakipata usumbufu wakati wa kusafirisha na kuuza mazao yao kwa kubambikiwa kodi nyingi. Hali hii inawarudisha nyuma wakulima badala ya kufaidika wanazidi kuwa masikini kwa kupoteza nguvu nyingi lakini hakuna wanachokipata.

Tangazo hilo toka kwa Rais wao limekuwa faraja na mkombozi mkubwa kwa wakulima wengi pamoja na wafugaji ambao Rais Magufuli amesema imefikia wafugaji walikuwa wanalipa kodi ya kwato kwa maana ya kila kwato ilikuwa ikilipiwa kodi.

Akiwa njiani kutoka Wilayani Kibondo kuelekea Wilaya ya Kasulu, Rais Magufuli alilazimika kusimama njiani kuzungumza na wananchi waliojazana kutaka kumsikiliza. Aliwaambia kuwa maamuzi aliyoyafikia naa kutangaza jana kuwa wakimbizi warudi nyumbani kwao kwa kuwa kuna amani sio kwamba anawafukuza bali ni ukweli kuwa wakimbizi wanachukua asilimia kubwa ya bajeti ya serikali katika mkoa huo.

“Kuna wakati wakimbizi katika mkoa wa Kigoma walikuwa wengi kuliko wananchi wa mkoa wa Kigoma. Huduma za maendeleo zilikuwa zikitumika kwa wakimbizi kuliko wananchi walengwa. Sasa Burundi ni shwari wakimbizi warudi kwao wakalime wale kwa jasho lao" amesema Rais Magufuli.

Akaongeza kuwa yeye hakuchaguliwa na Watanzania kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi wa Burundi bali amechaguliwa na mamilioni ya watanzania kwa ajili ya kuwaletea maendeleo watanzania na nchi yao kwa ujumla.

"Nilichaguliwa kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania sio kwa maendeleo ya wakimbizi" Rais Dk John Pombe Magufuli akiwa njiani Wilayani Kibondo kuelekea Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma

IMEANDIKWA NA SELEMANI NZARO- HABARILEO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post