Picha: DC SHINYANGA AKABIDHI SARE ZA SHULE KWA WATOTO WANAOISHI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU,AITAKA JAMII KUSAIDIA WATU WENYE MAHITAJIMkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amewataka wakazi wa mjini Shinyanga kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kupata elimu wakiwa katika mazingira rafiki na kupata ufaulu mzuri ambao utawafanya wafikie malengo yao ya maisha.

Matiro amesema anasikitishwa na wananchi mjini Shinyanga kuwa wa kwanza kuchanga michango ya harusi na wengine kutumia pesa hovyo kwenye vileo na wakati kuna watoto wanahitaji msaada hata wa sare za shule na viatu ili waende shule lakini kutokana na kuishi mazingira magumu watoto wanakwama na hatimaye kufanya vibaya darasani.

Matiro ametoa rai hiyo leo Alhamis Julai 6,2017 mjini Shinyanga wakati akikabidhi nguzo za shule kwa watoto 164 kati ya 1400 ambao wanaishi katika mazingira magumu katika manispaa ya Shinyanga.

Matiro ametoa msaada huo kwa kwshirikiana na Shirika la TVMC na PWWCO ambayo yanasaidia watoto na akina mama wanaoishi katika mazingira magumu mjini Shinyanga.

Matiro alisema lengo kuu la msaada huo kuuonesha umma kuguswa namna ya kusaidia watoto wanaoishi mazingira hayo na siyo kuiachia serikali peke yake zikiwamo NGO's na Wageni kutoka nje ya nchi kuja kuokoa watoto hao na wakati wananchi nao wana uwezo wa kuwatatulia changamoto hizo.

"Ukipita mchango wa harusi unakuta watu wanakuwa wa kwanza kuchangia tena kwa haraka lakini likija suala la kusaidia watoto wanaoishi mazingira magumu, kila mtu utasikia akisema hana pesa ,wananchi mnatakiwa mbadilike" alisema Matiro.

Naye mkurugenzi wa Shirika hilo la TVMC Mussa Jonas Ngangala alisema walifanya utafiti wa kubaini watoto wanaoishi katika mazingira magumu Aprili mwaka huu kwa kushirikiana na wenyeviti wa mitaa na watendaji katika kata zote 17 za manispaa ya Shinyanga ambapo walipata watoto hao 1400 na katika awamu ya kwanza wamesaidia watoto 164 huku wakitarajia pia kufungua kituo cha watoto wanaoishi katika mazingira magumu mjini Shinyanga.

Alisema changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili kwenye zoezi hilo la kutambua watoto wanaoishi katika mazingira magumu kuwa ni baadhi ya wenyeviti wa mitaa kugomea kufanya zoezi hilo kwa madai ya kutaka posho kwanza na hivyo kujikuta hapo mwanzo wakipatiwa watoto ambao sio wahusika ambapo waliwakataa na kufanya mchakato upya na kuwapata watoto sahihi.

Ngangala alisema zoezi la kutambua watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika kata ya Shinyanga Mjini liliaharishwa kwa sababu ya viongozi wa serikali za mitaa kutaka posho na kugomea zoezi hilo.

Kwa upande wake Ofisa elimu shule ya msingi manispaa ya Shinyanga Yesse Kanyuma alisema msaada wa nguo hizo utasaidia wanafunzi hao kufanya vizuri katika masomo yao ikiwa mtoto anaposoma katika mazingira magumu kamwe hawezi kufanya vizuri sababu akili yake haitakuwepo darasani na kuanza kuwaza wapi atapata chakula sambamba na mavazi yake kuchakaa na hivyo kumuhamisha kabisa darasani na kutomuelewa mwalimu.

Mkurugenzi wa Shirika la TVMC mjini Shinyanga Mussa Jonas Ngangala akisoma taarifa kwa mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro jinsi shirika hilo linavyosaidia watoto wanaoishi katika mazingira Magumu na malengo yao juu ya kusaidia watoto 1,400 wanaoishi katika mazingira magumu katika manispaa ya Shinyanga.
Mkurugenzi wa Shirika la TVMC mjini Shinyanga Mussa Jonas Ngangala akisoma taarifa kwa mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akigawa sare za shule kwa watoto 164 wanaoishi katika mazingira magumu katika manispaa ya Shinyanga.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akimkabidhi sare ya shule mwanafunzi.
Zoezi la kukabidhi sare za shule likiendelea
Mwanafunzi akipokea sare za shule
Zoezi la kukabidhi sare za shule likiendelea
Watoto 164 wanaoishi katika mazingira magumu wakiwa wamekaa wakisubiri kupewa msaada wa sare za shule na mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwa na mtoto anayeishi kata ya Ibadakuli na kusoma shule ya msingi Viwandani mjini Shinyanga ambaye anaishi katika mazingira magumu na bibi yake ambaye naye ni mgonjwa na amekuwa akigeuka kuwa mlezi wa familia ambapo akitoka shule anachukua panga na kwenda kuchanja kuni na kuuza ili apate pesa ya kula yeye na bibi yake, jambo ambalo lilimgusa mkuu huyo wa wilaya na kuamua kumchangishia pesa pamoja na kumtafutia wadau wa kusaidia familia yake ikiwemo chakula, afya ,mavazi na elimu sambamba na kukarabati nyumba ambayo anaishi na bibi yake.
Mtoto huyo akielezea historia ya maisha ambapo wadau waliguswa na kutoa misaada mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya Shinyanga Josephine Matiro akimkabidhi nguo za shule mtoto huyo ambaye anaishi na bibi yake,na yeye ndiye mlezi wake. Ofisa Utumishi wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga Magedi Magezi alitoa shilingi 30,000 kwa ajili ya kumnunulia viatu mtoto huyo.
Michango ya fedha ikiendelea ili kumsaidia mtoto ambapo jumla ya fedha Shilingi 195,600 zilipatikana pamoja na ahadi ya vyakula kila wiki na wengine kila mwezi kuahidi kusaidia familia hiyo
Mchungaji wa Kanisa la Wasabato mjini Shinyanga John Kilinda akitoa shilingi 300,000 huku Mwezake wa kanisa la Wasabato Lubaga Elias Nyangusu akiahidi kukarabati nyumba anayoishi mtoto huyo.
Mwenyekiti wa makanisa ya kipentekoste mkoa wa Shinyanga Askofu Elias Madoshi kutoka kanisa la FPCT akiahidi kuchukua watoto 10 ambao wanaishi katika mazingira hayo magumu na kuwasaidia kielimu na huduma zote huku akiahidi kutoa gunia la mchele kwenye familia ya mtoto anayeishi na bibi yake.
Naye mfanyabishara wa maduka ya nguo za kisasa mjini Shinyanga Ommy Fashion (aliyevaa miwani kulia) hakuwa nyuma kutoa mchango kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira hayo magumu ambapo alitoa shilingi 200,000.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akimkabidhi Ofisa Elimu kata ya Ibadakuli Alphonsina Sendaye fedha zilizochangwa na wadau na kutoa maagizo zitumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa kumsaidia mtoto huyo.
Wazazi na walezi wa watoto hao wakiwa eneo la tukio.
Wazazi ,walezi na viongozi mbalimbali wa serikali wakishuhudia tukio hilo la ugawaji sare za shule kwa watoto hao wanaoishi katika mazingira magumu. 

Picha zote na Marco Maduhu- Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post