DC NZEGA AWATAKA WANASIASA NA WANAHARAKATI KUPINGA TAFITI ZA KISAYANSI KWA TAFITI NA SIYO MANENO MATUPU


Mkuu wa wilaya ya Nzega Godfrey Ngulupa akifungua mafunzo ya Maafisa ugani Nzega-Picha na Hellen Isdory
Mratibu wa OFAB Tanzania Philbert Nyinondi akitoa Maelezo kwa Mkuu wa wilaya  ya Nzega.
Picha ya pamoja kati ya Mkuu wa wilaya ya Nzega na Maafisa Ugani wa wilaya ya Nzega
***

Mkuu wa Wilaya Nzega Godfrey Ngupula amewataka wanasiasa na wanaharakati kuacha kupinga kila tafiti za wanasayansi kwa maneno matupu badala yake wapinge tafiti kwa kutoa nao tafiti ili kuepuka kuleta mkanganyiko wa uelewa kwa wananchi.

Ngupula alitoa rai hiyo wakati akifungua Mafunzo kwa maafisa ugani 63 katika wilaya ya Nzega ,yaliyoandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Jukwaa la bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo(OFAB) yenye lengo la kuwakumbusha wagani hao namna ya kutumia kilimo cha kisasa chenye manufaa kwa jamii.

Ngulupa alisema ipo haja kwa wanasiasa kuwa na siasa safi na zisizo kuwa na athari kwa jamii hususani kuweka vipingamizi katika tafiti za wanasayansi jambo ambalo linaweza kuleta athari kwa jamii ikiwa sasa kuna uhitaji zaidi teknolojia mbalimbali hususani katika sekta ya  kilimo ambapo mabadiliko ya hali ya hewa pia  yanaathiri sekta hiyo.

"Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema mambo ya misingi ambayo jamii inatakiwa kujua kuwa ni pamoja na siasa safi, tuache siasa za maji taka kwani kitu cha kisayansi kinapingwa kwa Tafiti za kisayansi na si kupinga bila kujua wanachopinga",alisema.

"Wanansiasa wanatakiwa kuwasilikiza wanasayansi na kuelewa wanachosema kwani wana wajibu wa kuleta utafiti katika jamii na wao inatakiwa watunge sera kuangalia tafiti hizo na kuzifanyia kazi na si kila mwanasiasa kupinga tafiti za kisayansi kwa maneno tu”,aliongeza Ngulupa.

Aidha Ngulupa alisema hivi sasa anajitahidi sana wananchi wake wapate mazao ya chakula ili waweze kuepeukana na njaa hivyo wana uhitaji mkubwa wa mbegu ambazo zitaendana na hali ya hewa ya sasa.

“Mimi ni mwanasiasa na kiongozi wa wilaya lakini najua kabisa wananchi wakiwa na njaa siwezi kuwaongoza lakini mwenye njaa dawa yake siyo siasa ,kutokana na mabadadiliko ya hali ya hewa hapa wilayani wananchi wangu nimewasisistiza kulima mihogo,viazi vitamu,mtama pamoja na pamba ili kupata Pesa",alieleza mkuu huyo wa wilaya.

"Sasa mlipokuja na kunieleza kuwa kuna mbegu za Mihogo zenye kuhimili magonjwa pamoja na mbegu za mahindi za wema ambazo na mimi natamani kama kuzipata hizo mbegu katika wilaya yangu ili kuanza kuzitumia”,aliongeza.

Wilaya ya Nzega imesemekana bado ipo katika hali mbaya ya kilimo kutokana na hali ya hewa hivyo kwa sasa wanatumia kilimo cha mihogo tu katika kujipatia kipato na chakula jambo ambalo lina athari kwa jamii.
Na Hellen Isdory - Nzega

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post