ASKARI WA JWTZ AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA MAUAJI


Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Marwa Wambura amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni Dar es Salaam  akikabiliwa na shtaka la mauaji.

Marwa (25), ambaye ni askari wa Kikosi cha Jeshi namba 83 kilichopo Kiluvya amefikishwa mahakamani kujibu shtaka la kumuua Rashid Kashinde.

Akisoma hati ya mashtaka jana (Julai 5) Wakili wa Serikali, Joseph Nasua mbele ya hakimu Iz-Haq Kuppa amedai mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 196 cha Sheria ya Mwenendo wa Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

"Mshtakiwa unadaiwa Juni 17, 2017 ukiwa eneo la Kibamba CCM ulimuua Kashinde wakati ukitambua kwamba ni kosa kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," alidai Nasua.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Kuppa amesema mshtakiwa hapaswi kujibu kitu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo kisheria wa kusikiliza shauri hilo.

Kuppa amesema kwa mujibu wa sheria, kesi hiyo inatakiwa kusikilizwa katika Mahakama Kuu, hivyo itaendelea kutajwa hadi hapo upelelezi utakapokamilika.

Mshtakiwa alipelekwa mahabusu na kesi itatajwa Julai 18.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post