JINA LA KIJIJI 'ZUZU' LAMCHEFUA MIZENGO PINDA

WAZIRI Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amesema anafarijika kuona mchakato wa kubadilisha jina la kijiji cha Zuzu umeanza kwa kuwa jina hilo halina ustaarabu kulingana na maana yake halisi.

Alisema sasa wanakwenda kupata jina linaloendana na eneo hilo ambalo wanaishi wachapakazi wengi.

 Shamba la Pinda lililoko kijiji cha Zuzu ni moja ya miradi iliyotembelewa na Mwenge wa Uhuru juzi na kuwawezesha wakimbiza Mwenge kitaifa kushuhudia shughuli mbalimbali zinazofanyika katika shamba hilo ambalo pia linatajwa kuwa shamba darasa kwa sasa.

Alisema licha ya mafanikio mengi ambayo yamepatikana kilio chake ni jina la kijiji kuwa halina ustaarabu masikioni mwa watu. 

”Zuzu maana yake ni mpumbavu, silipendi jina hilo, sijui walitoa wapi nimekwenda kwenye mtandao nakuta jina ni Zinje kila nikiuliza sipati jibu lini walitubaini sisi ni mazuzu watu wazuri huku tunafanya kazi tunajiendeshea maisha yetu,” alisema 

“Nikamwambia mkuu wa mkoa jina hili si letu ila wametubambikiza tu. Hoja tunayo nadhani serikali imetusikia na tutapata jina ambalo linaendana na eneo hili,” alisema.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa, Amour Hamad Amour amewataka viongozi nchini kutekeleza kwa vitendo sera, mipango na mikakati ya kukuza uchumi badala ya kuhubiri na kuhimiza kwa wananchi bila wao kuonesha mfano. 

“Huu ni mfano ulio bora unaopaswa kuigwa na kila kiongozi mikakati ya kukuza uchumi katika nchi inatakiwa kutekelezwa kwa vitendo,” alisema.

Awali akitoa maelezo kuhusu shamba hilo, mke wa Waziri Mkuu mstaafu Pinda, Tunu Pinda alisema harakati za kuanzisha shamba hilo zilianza mwaka 2001 na shamba hilo lina ukubwa wa ekari 60. 

Alisema shughuli mbalimbali zimekuwa zikifanyika katika shamba hilo ikiwemo kilimo, ufugaji na huzalisha gesi ya asili ya biogas kwa ajili ya nishati ya kupikia na taa.

Alisema shamba hilo limekuwa likitumia mbolea ya samadi katika kilimo. Pia alisema shamba hilo lina mizinga 403 ya kisasa ambapo katika msimu wa mavuno uliopita kiasi cha tani 7.5 za asali zilipatikana. ‘’Bidhaa zinapatikana dukani kwa nembo ya Pinda Honey” alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments