WANAHABARI WASIO NA TAALUMA YA UTANGAZAJI NA UANDISHI WA HABARI LAZIMA WASOME



Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) ambaye ni Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas.
****
WASIO na taaluma ya Utangazaji na Uandishi wa Habari nchini, wanaofanya kazi kama watangazaji au waandishi wa habari katika vyombo mbalimbali vya habari, wametakiwa kutumia vyema miaka mitano waliyopewa kisheria kwa ajili ya kujiendeleza, ili kuepuka kutotambuliwa katika tasnia ya habari baada ya muda huo kuisha.

Aidha, wametakiwa kutopoteza muda kupiga kelele na kufanya mashauriano yasiyowasaidia kuhusu uamuzi huo wa kisheria, kwa sababu kiwango cha chini cha elimu ya mwanahabari kilichokwishaamuliwa kupitia Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 ni Stashahada ya Uandishi wa Habari na si uzoefu wa kuandika, ubunifu wala sauti nzuri ya kutangaza pekee.

Ushauri huo ulitolewa na wadau mbalimbali wa habari pamoja na wanazuoni Dar es Salaam jana, baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, kulieleza Bunge mjini Dodoma juzi kuwa asilimia 90 ya watangazaji nchini hawana taaluma ya Utangazaji wala Uandishi wa Habari, hivyo kusababisha weledi na maadili ya kazi hiyo kushuka.

Alisema hayo wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18. Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) ambaye ni Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas, alisema Sheria hiyo ya Huduma ya Habari imetoa fursa maalumu kwa watu wote wasio na taaluma ya uandishi wa habari kwenda shule kujiendeleza kufikia angalau kiwango cha chini cha elimu kinachostahili au kujiendeleza kufikia ngazi ya juu zaidi ya stashahada.

“Asilimia 90 ya watangazaji wasio na taaluma ni sehemu ya wanahabari walio katika vyombo vya habari vya kielektroniki, lakini wapo katika magazeti pia, hivyo si vyema kuiacha fursa hiyo ipotee kwa anayependa kuendelea kubaki katika taaluma ya habari baada ya muda huo kupita.

Kwa mujibu wa Dk Abbas, taaluma ya habari itaheshimika, weledi kukuzwa na maadili kuzingatiwa, ikiwa wanahabari watafikia viwango vya elimu vinavyokubalika katika tasnia hiyo, tofauti na ilivyo sasa ambapo baadhi ya watu wanafanya kazi ya kutangaza na kuandika habari bila kuwa na elimu yoyote ya Habari.

Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), Ayoub Rioba, alilieleza HabariLeo kuwa wasio na viwango vya elimu ya Habari vinavyotakiwa hawapaswi kuogopa kwenda kusoma, kwa sababu Uandishi wa Habari na Utangazaji ni taaluma inayompasa mtu kuwa na viwango vya elimu vinavyokubalika kisheria.

Alisema tofauti na ilivyokuwa zamani, utangazaji kwa sasa unachukuliwa kama ubunifu pekee unaotumika kuvuta watu, bila kuangalia misingi ya uandishi wa habari na maadili, yanayowalinda watangazaji na wananchi wanaofikishiwa habari hizo pia.

Dk Rioba alisema, “ubunifu pekee hautoshi, misingi ya Uandishi wa Habari na maadili vinahitajika pia, hivyo watu wasitafute mashauriano yasiyowasaidia katika hilo au kupiga kelele, bali waende kusoma na kuhakikisha wanapata elimu inayotakiwa ili wawe na weledi pamoja na maadili yanayotakiwa katika taaluma hiyo ya habari.

Kwa maelezo yake, kukosa elimu ya habari kunasababisha weledi na maadili kushuka, jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa masafa ambayo ni mali adimu, yatumike vibaya kwa mambo yasiyo ya msingi, hivyo kupotea bure au kutumika kwa ajili ya kuburudisha tu.

Alisema masafa yanapaswa kutumika kuelimisha watu masuala mbalimbali ya msingi yakiwemo ya afya, utunzaji wa mazingira na mengine yenye umuhimu kwa jamii. Naye Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Mfuko wa Tanzania Media Foundation (TMF), Ernest Sungura, alisema misingi ya taaluma ya habari lazima itambuliwe na nidhamu ya studio hasa za redio nayo isimamiwe vyema kuepusha matumizi mabaya ya muda pindi watangazaji wanapokuwa hewani.

Kwa maelezo ya Sungura, hilo litawezekana endapo wanahabari; waandishi wa kawaida, watangazaji na wahariri watakuwa na taaluma ya habari huku wakitekeleza wajibu wao kwa kufuata miongozo itakayowaeleza watangaze nini na wakati gani kwa ajili ya mamilioni ya watu wanaowasikiliza.

“Muda wa hewani ni mali, hivyo uheshimiwe. Katika kuzingatia weledi huwa inatakiwa miongozo inayopitia michakato yote muhimu na kukubalika. Uhariri nao udhibitiwe kuhakikisha kinachoenda hewani kina faida kwa watu.

Bila elimu ya taaluma ya habari hili huwa gumu kutekelezwa. Watu waende shule,”alisema. Kadhalika, Mwanazuoni Robert Mkosamali, ambaye pia ni Mchambuzi wa masuala ya habari nchini, alisema ni vyema wanaotaka kufanya kazi katika tasnia ya habari wakatumia muda wa miaka mitano waliopewa kusoma, ili wafanye kazi kwa weledi, maadili na waweze kujiamini pia.

Mkosamali alisema kuna athari mbaya kufanya kazi ya uandishi au utangazaji bila kuwa na taaluma hiyo kwa sababu uwezekano wa kukiuka misingi ya kazi, madili na kupoteza muda unaopaswa kutumiwa kutangaza mambo ya msingi kwa jamii.
Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post