Video- KAULI YA KITILA MKUMBO BAADA KULA KIAPO IKULU


Rais Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 05 Aprili, 2017 amewaapisha viongozi aliowateua kushika nyadhifa mbalimbali.

Hafla ya kuapishwa viongozi hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Moja ya viongozi walioapishwa ni Prof. Kitila Alexander Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Prof. Mkumbo aliyekuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mmoja wa wanachama wa chama cha ACT Wazalendo, baada ya kuapishwa aliongea maneno machache akimshukuru Rais Magufuli kwa kuuona umuhimu wake na kumteua kuwa katibu katika wizara hiyo.

Aidha amemuhakikishia Rais kuwa ataifanya kazi yake kwa weledi mkubwa na taifa litarajie matokeo makubwa katika utendaji wake.

“Kazi yetu na jukumu letu kubwa ni kuhakikisha kuwa sera ya umwagiliaji tunaitekeleza” alisema.

Vilevile aliongeza kuwa katika maisha yake yote akiwa mhadhiri, amekuwa ni mtu wa kuhoji maswali mbalimbali kwa serikali ili kuhakikisha kuwa wanafanya kazi yao kwa weledi.

“Maisha yangu yote mpaka hapa nilipo nimetumia muda wangu mwingi kuhoji na kuuliza maswali hasa kwa serikali. Nimepata fursa sasa ya kushiriki kikamilifu, badala ya kuhoji nina kazi ya kujibu maswali ya serikali. Mh rais nakuahidi kuwa nitajibu hoja mbalimbali za serikali”  alisema.

Viongozi wengine walioapishwa leo ni pamoja na Dkt. Ave Maria Emilius Semakafu kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Baraka Haran Luvanda kuwa Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Sylvester Mwakinyuke Ambokile kuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini na Bw. Charles Edward Kichere kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Hapa chini ni video ya Prof. Kitila Mkumbo akiongea Ikulu jijini Dar es salaam leo mara baada ya kuapishwa na Mh. Rais Magufuli.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post