SERIKALI YATAIFISHA KIWANDA CHA NYAMA TRIPLE 'S' SHINYANGA

Miezi mitatu baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuuagiza uongozi wa mkoa wa Shinyanga kumfutia usajili mwekezaji wa Kiwanda cha Nyama, Kampuni ya Triple S na badala yake watafute mwekezaji mwingine,hatimaye leo Jumatano Aprili 5,2017,serikali mkoani Shinyanga imekitaifisha kiwanda hicho. 

Kiwanda cha nyama kilichopo Old Shinyanga kilikuwa chini ya mwekezaji wa kigeni Triple ‘S’ tangu mwaka 2007 ambaye alitarajiwa kukiendeleza lakini miaka 10 sasa hakijawahi kufanya kazi. 

Serikali ilimuuzia kiwanda hicho mwekezaji huyo ili kukiendeleza kwa biashara ya kuchinja mifugo na kuuza nyama ndani na nje ya nchi ili kukuza uchumi wa mkoa wa Shinyanga na wananchi kwa ujumla lakini matarajio yakawa hasi. 

Akizungumza kiwandani hapo mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack amesema kiwanda hicho sasa kipo chini ya serikali baada ya mwekezaji wake kukiuka masharti na kukitumia kwa mambo yake binafsi. 

"Natamka kuanzia sasa kiwanda hiki kipo chini ya serikali na walinzi wote mliopo hapa mundoke jeshi la polisi ndiyo litakilinda mpaka pale tutakapopata mwekezaji mwingine ambaye atakuwa mwaminifu",amesema Telack. 

Telack amesema haiwezekani serikali ya awamu ya tano inataka Tanzania yenye viwanda lakini mwekezaji huyo amekuwa akikitumia kiwanda hicho kufanikisha mambo yake binasfi na mkoa kukosa mapato. 

Msimamizi wa kiwanda hicho cha Triple ‘S’ Samwel Kombe amekubaliana na maagizo hayo ya serikali na kudai kuwa atamfikishia taarifa mkurugenzi wake kuwa kiwanda kimechuliwa na serikali. 

Kiwanda cha nyama cha Old Shinyanga mkoani Shinyanga kilijengwa na serikali tangu mwaka 1975 kwa lengo la kuinua uchumi wa wafugaji ,mkoa, taifa na kupunguza tatizo la ajira kwa vijana lakini hakijawahi kufanya kazi tangu kijengwe na mwaka 2007 serikali ilimpatia mwekezaji Triple S lakini kimemshinda kukiendesha. 

Januari 12 mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliuagiza uongozi wa mkoa wa Shinyanga kumfutia usajili mwekezaji wa Kiwanda cha Nyama, Kampuni ya Triple S na badala yake watafute mwekezaji mwingine. 

Agizo hilo alilitoa Mjini Shinyanga wakati akiwahutubia wananchi wakati wa ziara yake ya kikazi iliyoambatana na sherehe ya kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. 

“Futeni usajili wa mradi wa Triple S, haiwezekani mwekezaji akashindwa kuendesha kiwanda kwa zaidi ya miaka 10 sasa halafu tuendelee kumkumbatia, tafuteni mwekezaji mwingine, mkishindwa semeni Serikali iweke hela, ili uzalishaji uendelee,” alisisitiza rais Magufuli. 

Aliongeza kuwa mwekezaji huyo amekuwa mbabaishaji kwani tangu kipindi yeye (Rais Magufuli) alipokuwa Waziri wa Uvuvi na Mifugo alimfahamu na alimpa maelekezo cha kusikitisha hakuna jambo aliloendeleza ikiwemo kuanza kwa uzalishaji. 

Na Marco Maduhu –Malunde1 blog
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack akiwa katika kiwanda cha nyama cha Old Shinyanga
Kulia ni msimamizi wa kiwanda hicho Samwel Kombe akiongea na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack na kumpatia maelezo kwanini mpaka sasa kiwanda hakijaanza kazi huku ndani yake kukiwa patupu hakuna hata machine za kufanyia kazi na kubaki jengo hilo kuwa kama gofu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post