TRA YAKAMATA MALI ZA LUGUMI

Kampuni  ya udalali ya Yono, imefanikiwa kukamata mali za wafanyabiashara wanaodaiwa kodi ya serikali inayofikia zaidi ya Sh bilioni 68.1. Operesheni ya kukamata mali hizo kwenye maeneo mbalimbali ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam imefanywa ndani ya wiki moja.
 
Katika operesheni hizo maofisa wa Yono wamekuwa wakishirikiana na maofisa wa Mamlaka ya Mapato(TRA), ambayo ndiyo imeipa kampuni hiyo kazi ya kukusanya kodi kwenye maeneo mbalimbali nchini.
 
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono, Scholastica Kevela, Yono imepewa kazi na TRA kukusanya madeni yake ya kodi kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani Njombe, Mbeya, Iringa na Zanzibar.
 
Aliwataka watanzania kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za kuleta maendeleo kwa kulipa kodi bila shuruti ili zipatikane fedha za kujenga miundombinu kama barabara, reli, shule, madaraja, hospitali na zahanati.
 
Kuhusu taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba hata baadhi ya mali za Kampuni ya Lugumi zimeshikiliwa, Mkurugenzi huyo alithibitisha kuwa habari hizo ni za kweli ambapo wanashikilia nyumba za kifahari za mfanyabiashara huyo.
 
“Mmeniuliza kwamba mmesikia nyumba za Lugumi zimefungiwa ni kweli, amefungiwa nyumba zake za kifahari na anadaiwa Sh bilioni 14, yupo mtu anaitwa Gm Dewji naye anadaiwa Sh bilioni 1.8, Kampuni ya ujenzi ya Mutluhan Construction anadaiwa Sh bilioni 45,” alisema.
 
Alisema wanaodaiwa wanapaswa kulipa madeni yao TRA ndani ya siku 14 na kwamba muda huo ukipita watapewa maelekezo na serikali kama ni kuuza mali hizo ili kufidia madeni yao.
 
Ofisa Mwandamizi wa TRA, ambaye hakupenda jina lake litajwe alithibitisha kwamba nyumba ya Lugumi iliyoko Upanga mtaa wa Mazengo inashikiliwa na mamlaka hiyo na ghorofa la kifahari lililoko Mbweni JKT, Dar es Salaam.
 
“Hakuna siri maana mkienda kwenye hizo nyumba mtakuta alama ambazo huwa Yono wanaweka kwa nyumba inayoshikiliwa, nendeni Upanga na kule Mbweni JKT mtakuta hizo nyumba tunazoshikilia,”alisema

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post