MUME AMUUA MKE WAKE KWA IMANI ZA KISHIRIKINA

Mtu mmoja katika kijiji cha Solwe wilayani Kwimba mkoani Mwanza anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kumuua mkewe kutokana na imani za kishirikina.


Tukio hilo limetokea tarehe 5/04/2017 saa 5 asubuhi ambapo mtu huyo anayefahamika kwa jina la Kumalija Kondolo Basu anadaiwa kumchoma mke wake na kitu chenye ncha kali sehemu za kichwani na shingoni upande wa nyuma na kupelekea kifo chake papo hapo.


Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alikuwa akiishi na mkewe nyumbani kwake kijiji cha Bagadu wilayani Magu lakini hivi karibuni alikwenda kwa wakwe zake wilayani Kwimba kuwasalimia yeye pamoja na mkewe.Kamanda wa Polisi Mkoa wa mwanza DCP Ahmed Msangi amesema kuwa siku ya tukio mtuhumiwa alibaki nyumbani na mkewe kwani wengine walikuwa wamekwenda gulioni kwasababu ilikuwa siku ya gulio.


Kwa mujibu wa Kamanda Msangi, inadaiwa kuwa baada ya mtuhumiwa kuona wanafamilia hawapo ndipo alimchukua mkewe na kuingia naye ndani na kisha kutekeleza kitendo hicho.


Amesema wananchi walitoa taarifa polisi kuhusiana na tukio hilo ambapo askari walifanya ufuatiliaji wa haraka hadi eneo la tukio na kufanikiwa kumakamata mtuhumiwa.


Amesema mtuhumiwa wa mauaji hayo amekamatwa na yupo katika mahojiano na jeshi la polisi, pindi uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post