MAASKOFU WALAANI UTEKAJI WATU NA KUUA ASKARI POLISI

Matukio ya utekaji watu na kupotea kwenye mazingira yasiyoeleweka pamoja na mauaji ya   polisi wanane mkoani Pwani, ni baadhi ya mambo yaliyotawala katika mahubiri ya mkesha na ibada za Sikukuu ya Pasaka katika maeneo mbalimbali nchini.


Maaskofu, wachungaji na mapadri wa makanisa mbalimbali katika ibada zao, walitumia muda mwingi kuzungumzia matukio hayo na kutahadharisha kuwa ni ishara mbaya ya kuporomoka kwa amani nchini.  

Viongozi hao wa dini wanayatazama matukio hayo kwa sura mbili, kwamba yanafanywa na binadamu walio hai na binadamu wafu ingawa ni hai.

Askofu Amani-Moshi
Katika mahubiri yake, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi mkoani Kilimanjaro, Isack Amani, alisema vitendo vya utekaji nyara, biashara ya binadamu, mauaji ya askari, ubakaji na ulawiti na mengine yanayofanana na hayo, ni dalili ya amani na utulivu wa nchi kupotea.

Akihubiri katika ibada ya Pasaka iliyofanyika kitaifa katika Kanisa la Askofu la Kristo Mfalme, mkoani Kilimanjaro, Askofu Amani alisema vimekuwapo vitendo vingi vya uhalifu vinavyoendelea kutokea nchini yakiwamo mauaji ya ukatili ya askari, utekaji nyara na unyanyasaji wa raia, hali inayoonyesha  kupotea kwa amani na utulivu nchini.

“Sasa majambazi wamefikia hatua ya kuua askari, hii ni ishara mbaya na wapo baadhi yetu wanashangilia. Inaonyesha kwamba ni makundi mabaya ya uhalifu tuliyo nayo kwenye jamii.

“Kwa lugha nyingine tunaweza kusema tunahitaji msaada kwa sababu hali si nzuri na inatishia amani, umoja na utulivu wetu.

“Amani na utulivu ni vitu ambavyo vinapaswa kuchochewa kama moto ila sasa naona mambo hayako sawa. Ni lazima wananchi pamoja na Serikali yetu tubadilike, tuichochee amani yetu,” alisema Askofu Amani.

Alisema pia kwamba kuendelea kufanyika biashara haramu ya binadamu ni jambo jingine linaloonekana kuchangia kuongezeka vitendo vya uhalifu.

“Biashara haramu ya biandamu huliingiza taifa lolote kwenye maafa mengi ya uhalifu kwa vile  watu wamekuwa wanakodishwa na kufanya uhalifu. Hivyo basi, ni lazima Watanzania tubadilike na kuishi maisha yenye staha.

“Mauaji ya vikongwe na watu wenye ualbino, ushirikina, chuki, ubinafisi na kulipiza visasi ni baadhi ya mambo yanayoonekana kuidhoofisha nchi, hivyo ni lazima Serikali na wananchi wabadilike kulinda amani na utulivu.

“Wananchi tuungane na Serikali kulaani mambo yote ya uhalifu yanayoendelea nchini, tuliombee taifa letu ili wananchi tuwe na umoja katika kupambana na matendo ya uhalifu na uovu wote, na mkumbuke amani ya taifa letu ipo mikononi mwetu,”alisema.

Askofu huyo aliwataka wanasiasa wote nchini,  waache ubinafsi kwa kufanya kazi za kuimarisha vyama vyao pekee na badala yake watumie muda huo kuwaletea wananchi wao maendeleo.

Katibu Mkuu -TEC
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Padri Raymond Sabba, alisema taifa linatakiwa kuombewa ili kuondokana na matatizo katika kipindi hiki cha mashaka ili mambo yanayojitokeza yasiendelee kutokea.

Akihubiri wakati wa mkesha wa Pasaka katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Dar es Salaam, Padri Sabba alisema kwa kiasi kikubwa yanayoendelea yanatakiwa kukemewa.

Alivitaja vitendo hivyo kuwa ni pamoja na mauaji ya kutisha, watu kutekwa nyara, ufisadi, uzembe wa viongozi, dawa za kulevya na kukosekana kwa haki.

"Tuliombee taifa katika kipindi hiki ambacho inawezekana kumekuwa na mashaka yakiwamo mauaji ya ajabu kwa watu wasio na hatia kama albino, vikongwe na kukosekana kwa haki.

“Kila mtu anapaswa kutambua kuwa hayo yote ni makaburi yanayopaswa kuondolewa kwa sababu hayampendezi Mungu kwa vile pia yanadhalilisha utu wa mtanzania.

“Wanaotenda matendo hayo  wakati mwingine si wapagani bali ni wenye dini wanaojitambulisha kuwa ni wakristo wakati matendo yao hayafai,”alisema Padri Sabba.

Aliwataka wakristo kuhakikisha wanaliombea taifa katika kipindi hiki ambacho kuna mashaka juu ya mambo mbalimbali ya kutisha yanayoendelea nchini.

Askofu Sylvester Gamanywa
Askofu wa Kanisa la BCIC lililoko Mbezi Beach, Dar es Salaam, Sylvester Gamanywa, alisema matukio yanayotokea nchiniyana sura mbili.

“Hayo yanafanywa na binadamu walio hai na binadamu wafu ingawa ni hai. Kwa kifupi, yanafanyika mambo ya ajabu na ya kusikitikisha na ya kuudhi wakati mwingine.

“Huwezi kutoa uhai wa binadamu kama kitu cha mchezo. Tumeshuhudia mauaji ya polisi waliouawa Kibiti na si hao tu wameshauawa wengi. Tusishangae hayo ni matendo ya watu waliokufa kiroho.

“Kwa mateso aliyoyapata Yesu, tungeweza kuua askari wote kwa mkupuo, lakini Yesu badala ya kuua, alisamehe.

“Unapoona watu wanafanya vituko, mfano wazee wanafanya zinaa na watoto waliowazaa, hao ni wafu, wamekufa kiroho.

“Mara nyingi kifo cha roho huanzia kwenye kinywa cha mtu ambako maneno yake yanaweza kutoa majibu kama ni hai au mfu.

“Kama mtu anatoa maneno ya chuki, fitina, uchonganishi ama kupandisha watu hasira, hizo ni dalili za mauti ndani ya kinywa chake,”alisema Gamanywa.

Alisema pia kwamba  licha ya kuwapo kwa mamlaka za dola nchini, bado mambo mengi yanayotendeka kwenye jamii yanadhihirisha mamlaka zimezidiwa kutokana na kuongezeka kwa maovu kuliko nguvu ya udhibiti iliyopo.

“Mfu wa roho yuko hai mwili, lakini utashi wa kufufuka ni hiyari yake mwenyewe. Majambazi, wazinzi, waongo na wachawi, wakiamua kusema Yesu fufua roho zetu tuwe viumbe wapya tutoke katika makaburi, wote wanaweza kufufuka na polisi wakakosa kazi,” alisema.

Askofu Gamanywa pia aliwashutumu baadhi ya viongozi wa dini kwa madai kuwa wamesahau wajibu wao na kufanya kazi ambazo hawajatumwa na Mungu.

“Sisi viongozi wa roho na hapa nawazungumzia wakristo, tunatarajiwa kuleta ufufuo wa roho za watu waliokufa, lakini tunafanya kazi nyingine ambazo hatujatumwa na Mungu.

“Matamko ya kukemea na kulaani ni staili ya wanasiasa, sisi tunayo mamlaka inatoka juu. Hivyo basi, maneno yetu yanatakiwa kuwa ni habari za ufufuo kwa wenye dhambi ambazo mamlaka za kawaida haziwezi kufanya bali Yesu pekee.

“Tukihubiri watu wakaacha maovu, watafanya kazi bila kusukumwa, wataacha kazi haramu na wataacha uvivu.

“Kama viongozi wa dini watashindwa kuwahubiria watu wakaacha kutenda maovu, basi kazi hiyo itakuwa imewashinda na itabidi wajiuzuru.

“Kama wewe ni mchungaji ama askofu halafu kuna watu wanaokufuata ibadani lakini bado ni waongo, wezi, wafitinishaji, ujue kazi imekushinda.

“Kabla hatujawaambia wanasiasa wajiuzuru, tunatakiwa tuanze sisi. Mimi natangaza sijiuzuru bali nitawaambia ukweli, kwamba Yesu Kristo amefufuka ni lazima umkubali na kumwamini ili ufufuke roho.

“We must speak the truth (lazima tuseme ukweli), hata kama kuna watu wana fedha nyingi na wanatoa sadaka kubwa ni lazima waambiwe ukweli,” alisema Askofu Gamanywa.

Askofu Mkuu KKKT
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fredrick Shoo, alisema matukio ya utekaji yanajenga hofu ya kutoaminiana ambayo si nzuri na ni hatari kwa nchi.

“Mambo haya yanahitaji uthibitishisho, hivyo ni vema uchunguzi ufanyike na ikithibitika hatua zichukuliwe kwa sababu yanazidi kuwatia hofu watu,” alisema.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Blaston Gavile, alisema mauaji ya askari wanane yaliyotokea wiki iliyopita mkoani Pwani, yanasikitisha na watu wanatakiwa wafunge kwa ajili ya kuliombea taifa.

Akitoa salamu za Pasaka katika Usharika wa Kanisa Kuu mkoani hapa, Askofu Gavile alisema kazi ya wakristo si kulalamika bali ni kumgeukia Mungu na kumuomba   aliepushe Taifa dhidi ya matukio ya utekaji, mauaji na mengine.

“Kazi ya wakristo si kulalamika mtaani kama ilivyo kwa mataifa mengine bali kazi yao kubwa ni kufunga na kuomba kwa ajili ya taifa.

“Tuendelee kuliombea taifa na Mkoa wa Iringa, tuseme Mungu yatosha kuendelea kusikia matukio ya ajabu ndani ya nchi yetu,” alisema Askofu Gavile.  

Naye Askofu mstaafu wa Dayosisi hiyo, Dk. Owdenburg Mdegella, aliwataka Watanzania kuacha kupoteza muda kujadili mambo yasiyo ya msingi badala yake wajikite kujenga nchi.

Askofu mstaafu wa Kanisa la Pentekoste (FPCT) mkoani Singida, Dk. Paulo Samweli, alitoa rai kwa madhehebu ya dini nchini, kuliombea taifa  liweze kuondokana na umwagikaji wa damu kwa Watanzania wasio na hatia wakiwamo  polisi.

Akihubiri katika ibada ya Pasaka  katika Kanisa la Pentekoste mkoani humo, Dk. Paulo alisema mauaji ya polisi wanane Kibiti, Pwani hayavumiliki na kila mtanzania anapaswa kuyakemea yasijirudie.

Dk. Paulo alisema jukumu la polisi ni kulinda Watanzania wa madhehebu yote na wasiokuwa na dini na mali zao.

“Tukianza kuwaua kwa ukatili namna hii, nani atatulinda?  Wewe ukimuua   polisi  ujue wazi kuwa unajiua wewe mwenyewe bila ya kujijua.

“Unyama huu haukubaliki mbele ya Mungu na kwa Watanzania wote, tuungane kuukomesha.

“Watu wasipofanya maombi vitendo hivyo vinaweza kusambaa sehemu mbalimbali nchini na matokeo yake nchi haitakalika tena.

“Shughuli za kumwabudu Mungu kwa uhuru mpana kama ilivyo hivi sasa zitakuwa ni ngumu na kujiletea maendeleo nako kutakuwa ni shida kutokana na kuwapo   viasharia vya uvunjifu wa amani,” alisema Askofu Dk. Paulo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post