DKT. WILBROAD SLAA KUJIUNGA CHAMA CHA WANANCHI - CUF?

Wakati mgogoro ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) ukizidi kutokota, Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahimu Lipumba anadaiwa kutaka kumvuta aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk. Wilbroad Slaa, kujiunga na CUF.

Madai hayo yameibuka baada ya kuwepo kwa mawasiliano ya karibu kati ya Prof. Lipumba na Dk. Slaa ambao kwa nyakati tofauti mwaka 2015, walijiondoa kwenye vyama vyao kipindi cha mchakato wa kusaka mgombea urais wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa).

Ingawa Dk. Slaa kaika mahojiano alikanusha habari za yeye kutaka kujiunga na CUF, lakini habari zinasema kuwa mawasiliano kati ya Prof. Lipumba amekuwa akihaha kumshawishi Dk. Slaa pindi atakaporejea nchini ajiunge na CUF na kushika moja ya nafasi za juu za uongozi.

Taarifa za kuaminika zilieleza kuwa mawasiliano kati ya Prof. Lipumba  na DK. Slaa yanalenga kuboresha safu ya uongozi wa chama hicho kwa kumpa wadhifa wa Ukatibu Mkuu au Umakamu Mwenyekiti licha ya kudaiwa kwenda kinyume cha Katiba iliyoanzisha CUF.

Kwa mujibu wa katiba hiyo, nafasi za juu za uongozi wa chama hicho zinatakiwa kuzingatia uwiano wa pande mbili za Muungano. Endapo mwenyekiti anatoka Bara, Katibu Mkuu atatoka upande wa pili wa Muungano.

Baadhi ya wana CUF wanaomuunga mkono Prof Lipumba wamekiri kuwa kumekuwa na mawasiliano ya wawili hao, huku wakisema hakuna anayejua kiini cha kuimarika kwa mawasiliano hayo wakati huu ambapo CUF imepasuka katika makundi mawili, moja likiongozwa na Katibu Mkuu Maalim Seif na jingine lipo chini ya Lipumba.

Msemaji wa CUF inayoongozwa na Maalim Seif, Mbarala Maharagande, amesema kuwa taarifa za kurudi kwa Dk. Slaa amezisikia  japo hajui atajiunga na chama gani.

“Labda wale watu wa Lipumba ukiwauliza wanaweza kukuhakikishia hilo. Kwa nafasi ya katibu itakuwa ngumu kwa sababu katiba yetu hairuhusu, lakini kuwa mwanachama anaweza. Nguvu ya Lipumba ilishapungua sana na wenye chama chao (wananchi) watakwenda kukichukua na kumtoa ofisini kwa hiyo kama anarudi Dk. Slaa kuja kuongezea nguvu upande huo inawezekana”. alisema Maharagande.

Akizungumza kwa njia ya simu, Dk Slaa aliyekuwa Mbunge wa Karatu alisema taarifa hizo si sahihi kwani alishaahidi kwamba hatarudi kwenye siasa za vyama.

Alisema hawezi kuyumba kwenye uamuzi wake licha ya kukataa kuweka wazi kwamba ni lini atarejeea nchini, alisisitiza kuwa msimamo wake wa kuachana na siasa za vyama uko palepale.

“Maneno yangu hayayumbi, sitafanya siasa za vyama, nimeachana nazo. Naomba msiniingize kwenye siasa uchwara, sizifanyi hizo… Saisa ni ajenda. Hizo siasa za kishabiki zifanyeni nyinyi huko Tanzania, mimi sifanyi ushabiki, hakuna mtu anayekula ushabiki, ndiyo maana siasa zangu siku zote ni ajenda, Watu wanataka maji, wanataka chakula, wanataka elimu bora, si ushabiki”

“Kwa miaka 20 niliyokuwa kwenye siasa sijawahi kufanya  ushabiki, nilitafuta ajenda na kuipanga mikakati kwa ajili ya wananchi” alisema Dk Slaa alipozungumza na mwandishi wa habari hizi.

Alisema atasimama kupiga kelele kwa ajili ya Tanzania pale atakapoona mambo yanakwenda kombo na atafanya hivyo kwa mustakabali wa Taifa si siasa.

Septemba 25, 2015 akizungumza na wandishi wa habari kwa zaidi ya saa 2 kisha kutangaza kujitoa Chadema, alisema ni afadhali apotee kwenye ulimwengu wa siasa duniani kuliko kumuunga mkono Lowassa.

Credit: TanzaniaDaima

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post