Serikali imepiga marufuku watu kufunga ndoa bila kuwa na cheti cha kuzaliwa kuanzia Mei Mosi, mwaka huu.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe amesema hayo jana Machi 16,2017 akiwa katika ziara yake mkoani Morogoro na kuongeza kuwa serikali imeamua kufanya hivyo ili kupata takwimu sahihi za wananchi wake zitakazosaidia kupanga mipango ya kimaendeleo sanjari na kuzuia wageni kuingia kinyemela nchini.
Pamoja na mambo mengine, Dk.Mwakyembe amewataka Wakala wa Usajili wa vizazi na Vifo (RITA), kuhakikisha inasimamia sheria ya usajili ambapo amesema kuwa bila kuwa na takwimu sahihi za vizazi na vifo ama ndoa inasababisha nchi kushindwa kusonga mbele kimaendeleo.
“Wenzetu nchi zilizoendelea suala la usajili wamelipa kipaumbele lakini sisi bado tuko nyuma, kwa mfano Mkoa wa Morogoro kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, inaonyesha kuna jumla ya wakazi milioni 2.2, lakini waliosajiliwa na kuwa na vyeti vya kuzaliwa ni asilimia 11 pekee huku wengine wakiwa bado hawasajiliwa,” amesema.
Dk. Mwakyembe pia ametumia nafasi hiyo kuwaonya watendaji wa mahakama watakaolalamikiwa na wananchi kufanya kazi kinyume na maadili ikiwamo upokeaji wa rushwa ama kutotenda haki na kutumia mahakama kugeuza kesi za madai kuwa kesi za jinai.