NI MTIKISIKO!!! ‘KUTEKWA’ KWA CLOUDS MEDIA MAZITO YAIBUKA,KILA MDAU ANA HASIRA

NA EVANS MAGEGE,
NI mtikisiko. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya tukio la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ‘kuteka’ Kituo cha Televisheni cha Clouds ambapo viongozi wa Serikali, wadau wamejikuta wakipishana kauli katika matamko yao.

Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli, kumkingia kifua Makonda  huku akipinga watu wanaotumia mitandao ya kijamii kumwelekeza nini cha kufanya.
Kutokana na hali hiyo kiongozi huyo wa nchi amemtaka Makonda aendelee kuchapa kazi na kamwe haongozwi na watu katika kufanya maamuzi yake.
Mbali na hilo wiki iliyopita Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, alitangaza kuanzia Mei Mosi mwaka huu, watu hawataruhusiwa kufunga ndoa bila kuwa na cheti cha kuzaliwa, tamko ambalo lilifutwa siku iliyofuata na Rais Dk. John magufuli.
Kauli hiyo ambayo Rais Dk. John Magufuli, alisema imemshangaza ya kupiga marufuku ufungishaji ndoa za aina zote bila kuwa na cheti cha kuzaliwa.
Wakati akiwa katika ziara yake mkoani Morogoro, Dk. Mwakyembe alisema Serikali imeamua kufanya hivyo ili kuwa na takwimu sahihi za wananchi wake ikiwa ni pamoja na kuiwezesha kupanga mipango ya kimaendeleo sambamba na kuzuia wageni kuingia nchini kinyemela.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita muda mfupi kabla ya kuondoka Ikulu ya Chamwino, Dodoma na kurejea jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli alisema kauli ya Dk. Mwakyembe kwamba Serikali imepiga marufuku ufungishaji ndoa za aina zote, iwe za kidini, kimila na kiserikali bila kuwa na cheti cha kuzaliwa kinachotolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) kuanzia Mei mosi, mwaka huu, ilimshtua hivyo alilazimika kutoa ufafanuzi na kuifuta.
Februari 12, mwaka huu, Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kuwaapisha baadhi ya watendaji akiwemo Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga, Rais Magufuli alitoa takwimu tofauti na zilizotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kuhusu idadi ya Watanzania waliokamatwa nje ya nchi na kufungwa katika magereza mbalimbali kwa kosa la dawa za kulevya.
Alisema Watanzania 1,007 walikamatwa ikiwa ni tofauti na idadi iliyotolewa na Waziri Mkuu wakati akihitimisha bunge la mwezi Februari ambapo alitaja idadi inayofikia zaidi ya 578.
Siku hiyo pia Rais Magufuli pasipo kutaja jina, lakini kauli yake ilijenga hisia kwamba huenda alimlenga Waziri wake wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alisema hakuna mtu anayehusika na dawa za kulevya ambaye ataachwa zaidi akisema anashangaa wengine wanasema kuna watu wamejenga majina yao kwa muda mrefu.
Kabla Rais hajatoa kauli hiyo, aliyesikika akitaka busara itumike kutokana na baadhi ya wasanii waliotajwa katika sakata la dawa za kulevya kutumia gharama kubwa kujijengea umaarufu wao ni Nape.
Agosti 26, mwaka jana  Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama machinga katika maeneo ya Kariakoo kwa sababu wanaleta usumbufu na uchafu.
Hata hivyo, Desemba mwaka huo huo, Rais Magufuli aliagiza wafanyabiashara hao wasibughudhiwe na wasiondolewe katika maeneo ya katikati ya miji wanayofanyia biashara kwani hakuna sheria inayowazuia.
Nape: Niko tayari kujiuzulu
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema kwamba yuko tayari kujiuzulu uwaziri kuliko kuvinyamazia vitendo vinavyonajisi uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Katika maelezo yake alisema matukio ya kunajisi vyombo vya habari yanatakiwa kupingwa hivyo kama akishindwa kusimamia hilo na yeye hafai kuwa katika nafasi aliyopo.
Nape alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati  alipotembelea Kituo cha Televisheni na Radio Clouds Media kwa lengo kusikiliza tuhuma zinazomlenga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye anadaiwa kuvamia kituo hicho Ijumaa ya wiki iliyopita.
Tuhuma hizo zinadai kwamba siku ya Ijumaa usiku akiwa na askari kadhaa wenye silaha nzito za moto Makonda alivamia kituo hicho cha televisheni kwa lengo la kuchukua video iliyorekodiwa ambayo haikuonyeshwa kwenye kipindi cha Shilawadu kama alivyokuwa amepanga.
Video hiyo yenye maudhui ya mwanamke mwenye mtoto mchanga ambaye anadai kutelekezwa na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambaye alidai kuwa ndiye baba wa mtoto.
Katika maelezo yake Nape alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko pamoja na vyombo vya habari hivyo akawahakikishia wanahabari kuwa ataulinda uhuru wa vyombo vya habari.
“Jambo hili linatisha kwa sababu halijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu na wala majirani zetu ukiacha pengine Burundi ambayo nilisikia wakati ule wanataka kumpindua Rais aliyepo madarakani. Hili ni jambo ambalo linatokea wakati watu wamefanya mapinduzi halafu wanavamia vituo vya utangazaji kutangaza mapinduzi yao,” alisema.
Alisema kwamba mtu anaweza kusema jambo hilo ni dogo lakini linaweza kusababisha utulivu wa miaka mingi wa nchi hii ukachafuka.
“Nimekuja kuwapa pole, lakini napenda kuwahakikishieni serikali ya Tanzania  ukiacha wale wanaoweza kutumia madaraka yao vibaya, serikali ipo pamoja na wanahabari na kuhakikisha uhuru wenu unalindwa…msiogope, timizeni wajibu wenu,” alisema.
Waziri Nape, alitangaza kuunda Kamati ya Uchunguzi yenye wajumbe watano wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dk. Hassan Abbasi ambayo itafanya utafiti kwa saa 24 na kumkabidhi ripoti leo mchana.
Alisema kamati hiyo ameiagiza ikamuhoji Mkuu wa Mkoa ili kupata ukweli wa kile kilichotokea na sababu iliyomsukuma kufanya tukio lile.
“Kesho mchana (leo) nitatoa matokeo ya utafiti uliofanywa na hatua tutakazozichukuwa, lakini msingi nawaombeni kama mlivyotulizana, endeleeni hivyo msiogope kukosoa kwa sababu Tanzania ni ya kwenu wala sio ya mtu mmoja mmoja ni ya kwetu sisi na watoto wetu na wajukuu zetu.
“Kama kunajambo haliendi sawa tukinyamaza ni sawasawa na kushiriki kutengeneza vifo vya watoto wetu na wajukuu zetu na ndugu zetu , hili si sawa kwa sababu ni dhambi kwa sisi wenyewe lakini ni dhambi hata mbele ya Mwenyezi Mungu,” alisema.
Alisema hawezi kupuuza jukumu la vyombo vya habari kuifanya nchi kuwa na amani na utulivu ni kubwa hivyo haiwezekani kupuuzwa hata kidogo.
Alisema kwa mtu yeyote ambaye anataka kuipupuuza jukumu la vyombo vya habari atapuuzwa yeye kwanza.
“Chini ya uwaziri wangu hakuna uhuru wa habari utakaovunjwa, itabidi tupambane tuhakikishe wale wasiotaka kuutambua na kuulinda uhuru wa habari tunashughulika nao.
“Yaani kwa uwekezaji wa miaka 20 Clouds wamekuwa nao anakuja mtu kutaka kuuharibu kwa dakika tano. Clouds Media ni brand kubwa katika nchi yetu huwezi kuja ukataka kuikanyaga kwa siku moja halafu unaipoteza hivi.
“Kitendo hiki kimenajisi uhuru wa habari kwenye nchi yetu, kimetia doa katika uso wa kimataifa, kama waziri mwenye dhamana ninao wajibu wa kuhakikisha tunasafisha doa hili kwa kuchukuwa hatua zinazostahili,” alisema Nape.
Kamati ya Bunge
Katika hatua nyingine Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilitembelea kituo hicho cha televisheni na redio na kupata wasaa wa kuzungumza na uongozi wa kituo hicho kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari.
Baada ya mazungumzo ya ndani na uongozi wa kituo hicho yaliyolenga kupata ukweli wa tukio zima alilolifanya Makonda, Mwenyekiti wa Kamati hiyo,  Peter Serukamba alikemea vikali kitendo hicho.
“Sisi kama Kamati ya Bunge,  Spika alituomba tuje tuone kilichotokea, tumekutana na uongozi wa Clouds Media na wametuambia yaliyotokea. Kwa niaba ya Kamati tunawapa pole wafanyakazi wa Clouds lakini hii ndiyo kazi ya uandishi wa habari na hii ndiyo mitihani yake,” alisema.
Alisema jambo hilo ni fundisho kwa wanahabari kuwa wasikubali kutumiwa na wanasiasa. Aliongeza kwa kusema kwamba inawezekama matokeo ya jambo hilo yamesababishwa na wanasiasa kutengeneza ujamaa na baadaye kulazimisha mambo ambayo ni nje ya utaratibu.
Pia aliongeza kwamba alichofanya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni matumizi mabaya ya madaraka aliyopewa.
“Kulinda Taifa letu, haiwezi kuwa mtu mmoja kwa sababu anavyombo anaweza akafanya jambo ambalo analitaka hili halikubariki…leo amekuja kwenye vyombo vya habari, kesho atakwenda kwenye migahawa, kesho kutwa atakwenda kwenye nyumba zetu , niwaombe sana vyombo vya ulinzi na usalama fanyeni kazi kwa mujibu wa sheria zilizowaweka madarakani…nchi hii inaongozwa kwa sheria na jambo hili ni gumu sana kulifikiria lakini  kunakulewa madaraka ,” alisema.
Sugu
Naye Waziri Kivuli wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Joseph Mbilinyi(Sugu), alisema kitendo kilichotokea kinastahili kulaaniwa.
Aliongeza kuwa hii sio Tanzania ambayo wananchi walikuwa wanaitarajia.Alisema uvamizi uliofanywa na Makonda kwa Clouds linatoa tafsiri ya kuhoji kuwa nchi inakwenda wapi.
Bashe
Kwa upande wake mjumbe wa kamati  hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM),  alisema tasnia ya habari hapa nchini imejengwa kwa muda mrefu.
Alisema wabunge kwa upande wao wanajukumu la kuhakikisha mhimili wa Serikali unatimiza wajibu wake.
“Makonda kama kijana mwenzangu ambaye siku zote amekuwa akifanya kazi nzuri sana tangu wakati akiwa Mkuu wa Wilaya mpaka kawa Mkuu wa Mkoa, anafanya makosa ya kimkakati kila kukicha kumharibia uhalali wake katika umri hili ni jambo la hatari sana.
“Lakini naamini Serikali imeunda tume na kesho (leo) itatoa taarifa hivyo tusubiri kauli ya serikali itakayotolewa na ninaamini kistaarabu Paul Makonda sio dhambi ukikosea ukaja hadharani ukaomba radhi.
“Makonda anawajibu wa kuja akawaomba radhi Clouds kwa kitendo cha kuingia akiwa na askari waliokuwa na silaha na kutengeneza taharuki hii. Ni wajibu wa kiongozi yeyote unapokosea kuwaomba radhi uliowakosea,” alisema Bashe.
Dk. Mengi
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo Vya Habari Tanzania(MOAT), Dk. Reginald Mengi, alisema kuwa amesikitishwa na kitendo hicho.
Alisema yeye kama baba baada ya kusikia tukio hilo aliona ni muhimu kwenda kuwaona watoto wake.
“Nimekuja hapa kuwahakikishia watu wengine kwamba wasidhani nyie ni yatima, wakiwachezea wajue wamemchezea pia baba na katika hili tuko pamoja na wanaodhani wakivamia Clouds na kuiangusha watakuwa wameshinda lakini kabla ya kuiangusha Clouds tunatakiwa tupigane sana.
“ Nguvu yetu kama vyombo vya habari sio kituo kimoja kimoja bali wote tuko pamoja, mtu akigusa mmoja wetu mjue ametugusa wote na nilikuwa namwambia Waziri Nape kwamba wasituchezee maana tukiungana hivi watababaika sana,” alisema Dk. Mengi.
 Chanzo-MTANZANIA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post