MAHAKAMA YAWAACHIA HURU WATUMISHI WA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA - TFF

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru watumishi wawili wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Martin Chacha na Juma Matandiko  baada ya kuwaona hawana kesi ya kujibum. Uamuzi huo umetolewa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Akisoma uamuzi huo, Hakimu Shahidi amesema kuwa amewaachia huru washtakiwa baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi saba wa upande wa mashtaka na kuona upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa washtakiwa wametenda kosa.

Washtakiwa Matandika na Mecky wanatuhumiwa kwa kuomba rushwa ya Shilingi milioni 25.

Awali ilidaiwa kuwa Februari 4 mwaka jana, washtakiwa hao wakiwa waaajiriwa wa TFF walishawishi kuomba rushwa ya kiasi hicho cha pesa kutoka kwa Salum Kulunge na Constatine Morandi ambao ni maofisa kutoka Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Geita na Klabu ya Mpira wa Miguu Geita.

Ilidaiwa kuwa watuhumiwa hao waliomba rushwa hiyo kama kishawishi kwa TFF na Idara ya Uhamiaji Tanzania kutoa uamuzi dhidi ya klabu ya Mpira wa Miguu Polisi Tabora ili kuisaidia klabu  ya Geita kupanda katika ligi kuu ya Tanzania.
 
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Shahidi alisema katika ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka unaonesha hakuna mtu aliyeenda Takukuru kulalamika juu ya washtakiwa kuomba rushwa zaidi ya sauti ya CD kusambaa katika mitandao.

Amesema upande wa mashtaka haukuonesha kama kweli washtakiwa walitoka Geita kuja Dar Saalam.

Kuhusu sauti zilizotambuliwa za Mecky na Matandiko kupitia CD, Hakimu Shaidi amesema watu wana sauti za kufanana na hata kuigizana hivyo hauwezi kujikita kwenye ushauli kuwa ni washtakiwa wenyewe ndio wanaosikika kwenye hiyo CD.

Amesema, ni wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha pasipo kuacha mashakama kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo.

Hakimu Shahidi ameenda mbali na kueleza kuwa kwa mujibu wa ushahidi ulitolewa mahakamani hapo, imedaiwa kuwa kanuni za TFF zinaeleza wazi kuwa, mchezaji akibainika kudanganya ndiye anayepaswa kuadhibiwa lakini si timu kunyang'anywa pointi.

"Hawa hawakuwa na mamlaka ya kunyang'anya pointi, hivyo wasingeshtakiwa kwa kuomba rushwa na hata kama walitenda kosa basi wangeshtakiwa na tuhuma zingine, labda utapeli", amesema.

Kutokana na upungufu wa ushahidi, Hakimu Shaidi aliwaachia huru washtakiwa kwa sababu hawana kesi ya kujibu.

Kesi hiyo ilikuwa inaendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),Leonard Swai.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post