KAHAMA WATAKA UGORO UZUIWE KAMA VIROBA

KUTOKANA na serikali kupiga marufuku kuuzwa kwa pombe zenye vifungashio vya plastiki (viroba) kuanzia jana, baadhi ya wananchi mjini Kahama wameipongeza hatua hiyo na kuiomba pia ihamishie nguvu pia katika kupiga marufuku ugoro ambao umekuwa ukitumiwa na vijana wengi wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, baadhi ya vijana mjini Kahama wameipongeza serikali kupiga marufuku pombe hiyo huku baadhi yao wakishauri kuwa nguvu kubwa sasa ielekee katika kupiga marufuku matumizi ya ugoro ambayo ni makubwa na yanaweza kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

Walisema aina hiyo ya kilevi ya ugoro ambayo ilikuwa ikitumiwa na vijana katika kiwango cha chini katika siku za nyuma, lakini kwa sasa matumizi yake yamekuwa makubwa kutokana na mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanayofanywa na serikali.

“Tunaomba serikali iangalie kwa upande wa pili ambao ni matumizi ya ugoro ambao kwa sasa imekuwa ni tatizo kubwa kwa vijana baada ya kupambanza moto kwa dawa za kulevya kunakofanywa na Serikali. Kwa sasa dawa hizo hazipatikani kwa urahisi,” alisema mmoja wa wakazi wa Kahama, Selestine Bitende.

Alisema biashara ya ugoro ambayo imeibuka katika maeneo mbalimbali nchini, imekuwa ikiwapatia kipato kikubwa wauzaji kutokana na watumiaji wake kuwa wengi kwa sasa hali ambao kwa siku za baadaye inaweza ikaleta matatizo makubwa kwa vijana kama ilivyo kwa dawa za kulevya.

Bitende aliongeza kuwa wanaiomba serikali kupitia vyombo vya habari kuhakikisha kwa matumizi haya ya ugoro kwa vijana yanatokomezwa kama ilivyo kwa vita vingine ili kujenga Taifa la Vijana ambao wanaweza kulitumia Taifa katika siku za baadaye.

Edward Charles alisema suala la vijana kuvuta ugoro kwa sasa linafaa kukemewa kwa hali ya juu kwani hali ni mbaya kwa baada ya serikali kupambana na dawa za kulevya vijana hao wamehamia katika utumiaji wa ugoro.

“Unakuta mtu amebandika kibao katika mti kuwa ugoro mkali unapatikana hapa, ni lazima kutakuwa na mchanganyiko aidha wa madawa ya kulevya au vitu vingine kwani kwa uhalisia kilevi aina ya ugoro, pia kina ukali kama ilivyo kwa madawa ya kulevya mengine,” alieleza Charles.

Hivi karibuni, serikali ilitangaza vita dhidi ya dawa ya kulevya pamoja na wauzaji wake huku baadhi ya vijana waliokuwa wakitumia dawa wakionekana kuathirika kutokana na kutopatikana kwa urahisi kwa sasa hali iliyowafanya kuhamia katika kilevi kingine aina ya ugoro ambacho kinapatikana kwa urahisi tofauti na ilivyo kwa dawa za kulevya.

Na Raymond Mihayo- Habarileo Kahama

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post