WEMA SEPETU : NIMEVAA GWANDA TAYARI KWA MAPAMBANO



ALIYEWAHI kuwa mrembo wa Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu, amekihama rasmi Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Wema aliyekuwa mmoja kati ya wanachama maarufu katika kundi la wasanii wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka juzi kwa kaulimbiu ya ‘mama ongea na mwanao’ akiwa kama kiongozi wa wasanii, alishiriki kumnadi Mgombea Mwenza wa CCM ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassani, alisema kwa sasa ameamua kuvaa magwanda na yupo tayari kwa mapambano.

Akizungumza nyumbani kwao Sinza, Dar es Salaam jana, alisema amechukua uamuzi wa kuhama chama hicho baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kumtaja katika orodha ya watu wanaotumia dawa za kulevya na kusema kitendo hicho kilimdhalilisha.

“Nimeamua kufanya uamuzi wa kuhama CCM na sasa nahamia Chadema, sitaki nionekane labda nimepata hasira kulingana na tuhuma zinazonikabili, lakini nataka nionekane nimefanya uamuzi kama binadamu yeyote angeweza kufanya.

“Nimekubali na nimekiri kwamba nilisema nitakufa nikiwa CCM lakini ya Mungu mengi, natamani ningejua awali, nasema sijachelewa, naamini uamuzi wangu nilioufanya ni sahihi na nimeingia kwenye vita, nipo tayari kupigana, nina imani kwamba kutakuwa na watu wengine wapo nyuma yangu wengi watanifuata,” alisema.



Wema aliyekuwa na mama yake mzazi Miriam Sepetu ambaye na yeye alitangaza kuhama CCM na kuhamia Chadema, alisema alipokuwa kada wa CCM alikuwa mwaminifu na kwa kipindi chote alikipigania kwa uwezo wake wote.



“Nimetuhumiwa hivi karibuni na nilivyokuwa kama kada nilijitoa maisha yangu, utu wangu, nilipoteza muda wangu kupigania kile ambacho nakiamini ni sahihi lakini siku moja kisinitupe na kinithamini kwa kile nilichokifanya lakini tofauti na nilivyokuwa natarajia havikutokea.

“Sisemi kama nilikuwa nafanya ili nije kubebwa kama princess (binti wa mfalme) ama queen (malkia) kwa sababu Wema ulikuwa unajitoa basi hata ukikosea usiadhibiwe au ukiwa unatuhumiwa usichukuliwe hatua, hapana, sijamaanisha hivyo,” alisema.

Pia alisema baada ya kushutumiwa aliamua kukaa kimya muda mrefu kwa kuwa alikuwa anatafakari alipokuwa amekosea.

“Nimekaa kimya muda mrefu si kwamba nimefurahia kilichotokea, nilikuwa bado natafakari na kutathmini where did I go wrong (wapi nilikuwa nimekosea), ni kitu gani ambacho nimekosa na kufanyiwa hichi nilichofanyiwa, nilichogundua ni kitu ambacho najua mwenyewe siwezi kusema nafurahia,” alisema.

Wema alisema kitendo cha kutuhumiwa bila wahusika kuwa na uhakika na tuhuma kimemnyong’onyeza na kumvunja moyo kwa kiasi kikubwa.

“Wanasema wenyewe tenda wema nenda zako usingoje shukrani, lakini siku ya mwisho siwezi kuwa mnyonge kwa sababu naamini there is something called democracy (kuna kitu kinaitwa demokrasia) katika nchi yangu na hicho ndicho nataka kukipigania,” alisema.



Wema aliendelea kusema kuwa uamuzi aliouchukua ni mgumu lakini hatarudi nyuma na anaamini kuna kundi kubwa la watu wasiopungua 500 watamfuata.

“Huu ni uamuzi mgumu kidogo na wanasema uamuzi mzito lakini nasema there is no turning back (sitarudi nyuma) kama nimeamua, nimeamua na leo (jana) hii mnanirekodi haya yatakuwa ni maneno ambayo yatakuja kunisuta.

“Sidhani kama kuna mtu anapenda uonevu, sidhani kama kuna mtu anapenda kunyong’onyezwa, dola ibaki ifanye kazi yake kama dola hakuna aliyekataa na wala sipo kwa ajili ya kukataza dola kufanya kazi yake, ifuate sheria zake kama dola lakini tuangalie misingi ya haki za binadamu na watu,” alisema.

Pia alisema ameamua kuhamia Chadema kwa sababu ni moja ya chama chenye nguvu baada ya kuwapa shida wakati wa kampeni za uchaguzi.

“Nimeamua kuingia Chadema kwa sababu nimefanya utafiti wangu kwa muda mrefu hata tulipokuwa tunaipigania CCM, chama pinzani kilichokuwa kinatupa tabu ni Chadema na ningejua before (kabla) ningeshahamia zamani lakini ndiyo kutokujua sisi sote ni binadamu tunakosea,” alisema.

Alisisitiza kuwa Chadema ni chama kinachosimamia uhuru wa watu, kinapigania demokrasia anayohitaji ndani ya nchi.

“Ninachokitaka katika nchi yangu ni demokrasia, sitaki kingine, nataka kupigania uhuru wa watu, naamini kuna watu wengi nje ambao wapo katika hali kama niliyokuwa nayo mimi lakini wanaogopa kutoka na kufanya uamuzi.

“Ndiyo maana nimehamia people’s power, naamini katika nguvu ya umma, tunaweza tukaitengeneza Tanzania yetu ambayo tumekuwa tukiikosa muda mrefu, I’m proud to be Chadema member (najivunia kuwa mwanachama wa Chadema),” alisema.

Pia alisema kuna wengi wapo CCM wanafanyiwa mambo yasiyofaa lakini wanashindwa kujitangaza kwa umma kama wamechoka na kitu fulani.

Alisema hali hiyo inatokana na mazoea yaliyopo katika vyama jambo linalozaa matatizo makubwa na hakuna mtu anayeweza kulimaliza hilo kama wenyewe hawajaamua.

Alisema hajahama chama kwa hasira isipokuwa amekasirishwa na kitendo chao cha kukaa kimya alipopata matatizo.

“Ningetaka kuhama kwa hasira ningehama nilivyokosa ubunge, sasa hivi kwa sababu ya hizi tuhuma zilizotokea na chama kukaa kimya nilikuwa nadhani kwa fadhila ndogo kwa hili janga ningeonyeshwa hata huruma.

“Mimi nina mchango wangu mkubwa katika CCM, lakini hawakunijali hata wasanii walitishwa na kunitenga, nikajikuta nipo peke yangu ndiyo maana nimesema nimeonewa,” alisema.

Wema aliendelea kusema alipokuwa CCM alijitoa kwa kiasi kikubwa katika kazi za chama jambo lililotaka amwagiwe tindikali wakati wa kampeni.

“Nilikuwa nimejitoa, nilikuwa tayari kufa, niliponea chupuchupu kumwagiwa tindikali na wanachama wa CUF, walinimwagia michanga na maji ya moto, wakati nipo ndani ya gari nilikuwa nasikia wanasema wana tindikali tummwagie wapi, lakini leo hii pamoja na kuniweka ndani kwa tuhuma za uongo, hawakuwa na vithibitisho. “Mimi nilikaa zaidi ya wenzangu niliyoingia nao, kama chama kilinifanya nijisikie hivi kwanini niendelee kukaa, kwanini niwe karibu na watu ambao ulifikiri watakubeba wakati wa matatizo, wanasema mapenzi nipe nikupe bwana sio upande mmoja ikiwa hivyo yanakuwa sio mapenzi,” alisema.

Pia alisema hajapokea fedha yoyote kutoka Chadema au kushawishiwa kujiunga kama inavyotangazwa katika mitandao ya kijamii.

“Kama nimechukua hata shilingi 10,000 kutoka Chadema, kaburi la baba yangu Zanzibar naomba lititie na uingie ufa mkubwa, mambo ya fedha tumezoeshwa kwa CCM ndio wanavyofanya, mimi nikiamua kitu sirudi nyuma hii ni battle (vita), nipo tayari kupigana nadhani wapo watu wengi nyuma yangu kwa ajili ya demokrasia nitafanya tu,” alisisitiza.

Alisema kwa sasa nchi imeanza kupoteza demokrasia iliyozoeleka na huenda ikafika katika eneo ambalo haipaswi kuwapo.

Alisema tangu alipofanya uamuzi wa kuhama chama ameshindwa kuingia katika mitandao ya kijamii na alikuwa akitaka kutoa picha zenye nembo ya CCM kwa sababu ya vitisho.

“Mimi ningepokea dola laki mbili sijui ningekuwa wapi, tangu nilivyofanya uamuzi sijakaa na simu yangu, nilitamani kuingia Instagram tangu jana (juzi) kutoa kapicha cha CCM nilichokituma, kumekuwa na vitisho vya hapa na pale usifanye hichi kitakutokea ndiyo maana nasema kama vita nimevaa magwanda nipo tayari kupigana,” alisema.

Kuhusu madeni ya wasanii wanayoidai CCM, alikiri uwepo wa deni hilo na kusema kwamba hawezi kulizungumzia suala hilo kwa undani kwa kuwa kila wanapoenda CCM kudai fedha zao wanaambiwa wamfuate Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

“Wakati tunazunguka kuna madeni ambayo wasanii wenzangu wengi wanadai nikiwemo mimi, sitaki kuambiwa nakumbuka shuka asubuhi kwa sababu nimehama ndiyo naanza kukumbushia madeni, watasema nazungumzia fedha.

“Madeni yapo na wasanii wenzangu wengi tunadai, lakini tumeambiwa tumfuate JK, kila tukikumbushia tunaambiwa tukamdai JK na sasa kuna maneno mengi fununu fununu tu, tunasikia chama kama chama kina mambo mengi,” alisema.

Kwa upande wa mama yake Wema, alisema tangu mtoto wake alipokamatwa waandishi wa habari walikuwa wakimuuliza maswali mbalimbali hakuweza kuyajibu kwa sababu ya kutumia muda mwingi kutafakari suala la kuhama chama.

“Kwa muda mrefu waandishi mlikuwa mnasema mnasubiri nitoe mapovu, mimi huwa sitoi mapovu kuna gazeti wanasema mwanawe yupo ndani lakini haongei mimi huwa sishindani.

“Siku zote uchungu wa mwana aujuaye mzazi, nimehangaika na mwanangu alivyowekwa ndani na Makonda kashutumiwa anauza na kuvuta dawa za kulevya, mvuta dawa za kulevya anakaa hivi, kwanza zile siku saba alizowekwa tungemtoa kule hoi na alosto, CCM sijamwona mtu wala kunipa pole zaidi ya viongozi watatu waliopiga simu,” alisema Mama Wema.

Pia alisema wakati Makonda alikuwa akimtumia Wema vitu mbalimbali katika mitandao kwa ajili ya kumtangaza alikuwa hajui kama ni mvuta unga.

“Mwanangu amedhalilishwa, ameteswa hadi usiku wanafuatwa na Makonda huyu ambaye ana visa naye hatuvisemi leo alikuwa anamfanyia kazi atume kwenye mtandao kumbe anamtuma mvuta unga,” alisema Mama Wema.

Pia alisema utaratibu uliotumika kumtuhumu Wema haukuwa sahihi na haukufuata haki za binadamu.

Kwa upande wake, Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, aliyepokea kadi zao za CCM alisema wanaamini ujio wa Wema na mama yake ndani ya Chadema ni sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Na Aziza Masoud-Mtanzania Dar es Salaam

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527