WEMA SEPETU NA WENZAKE WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA DAWA ZA KULEVYA

wema sepetu
Sakata la Madawa ya kulevya limeendelea kugonga vichwa vya habari wiki hii ambapo Jumatatu hii Jeshi la polisi limedai toka lianze operesheni hiyo tayari limewakamata watuhumiwa 112 na kati ya hao 12 wamepandishwa mahakamani Jumatatu hii kwa ajili ya kiapo cha kutorudia matumizi ya Madawa ya kulevya baada ya kukiri kutumia.

Kati ya watu hao 12 ni pamoja na Wema Sepetu, Romy Jones, Petit Man, TID pamoja na wengine.

Aidha Wema Sepetu baada ya kiapo hicho atarudishwa polisi kwa ajili ya kuandaliwa shtaka jipya linalomkabili la kukutwa na msokoto wa bangi nyumbani kwake.

Akiongea na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema watuhumiwa wengi waliohojiwa walikiri kutumia Madawa ya kulevya na kati ya hao walieleza watu ambao wanawauzia.

“Tumewakamata watuhumiwa jumla 112 na tumekamata kete 299 zinazodhaniwa ni za Madawa ya kulevya na kwa kawaida haya Madawa Mkemia Mkuu wa serikali yeye ndiye atakayetuambia ni Madawa ya aina gani,” alisema Kamanda.

Aliongeza, “Katika watuhumiwa 112, kuna watuhumiwa 12 tumewapeleka leo mahakamani, tumewapeleka mahakamani kwa sababu sheria ya mwenendo wa mashtaka iko wazi kifungu cha 73 na 74, huwa tunaweza kuomba kwa mweshimiwa hakimu kuwaombea watuhumiwa kwa kiapo, kwamba hawa watuhumiwa tunataka wabadilishe tabia zao. Tunawapeleka mahakamani ili wakae chini ya uangalizi wa jeshi la polisi na mahakama kwa muda wa miaka 2 wasifanye makosa tena,”

“Kwa sababu tulichokibaini kwa wote tuliowakamata wengine wanakiri na wamekwenda kuonyesha hayo Madawa ya kulevya. Kwa hiyo kusudio la kwanza wawe chini ya uangalizi wetu, na kusudio la pili la kiapo chetu waache hiyo tabia ili wabadilike wawe raia wema, lakini la tatu tumeomba wale wanakuja kuripoti kituoni angalau mara mbili kwa mwezi na lengo letu ni kuona hawa ndugu zetu ambao walikuwa wanavuta madawa ya kulevya wameacha kabisa,”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post