WAZIRI LUKUVI AMNYANG'ANYA ARDHI MAKONDA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametangaza kumchukulia hatua mfanyabiashara wa Dar es Salaam, Mohamed Iqbal aliyempa Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda eneo la ukubwa wa ekari 1,500 ili kujenga viwanda vidogo, wakati linamilikiwa na serikali na si mali ya mfanyabiashara huyo.

Jumanne iliyopita mfanyabiashara huyo alimkabidhi Makonda eneo la ukubwa wa ekari 1,500 Kigamboni, kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo vya wafanyabiashara.

Ekari hizo zilitolewa na Kampuni ya Azimio Estate inayojihusisha na ujenzi wa majengo na uendelezaji wa ardhi na kukabidhiwa kwa Makonda.

Kampuni hiyo pia iliwahi kutajwa katika ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu ushiriki wake katika miradi ya ujenzi wa nyumba za Shirika la Tafa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambao unadaiwa uligubikwa na ufisadi.

Alipotembelea eneo hilo lililopo Kigamboni, Makonda aliipongeza kampuni hiyo kwa kukubali kutoa eneo lao na kusema wameonesha nia ya kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za nchi kuwa ya viwanda, hasa kwa kuwa wenye viwanda vidogo wana changamoto nyingi za maeneo na wengine kulazimika kuweka katika maeneo ya watu.

Mkurugenzi wa Azimio Estate, Iqbal alisema baada ya kupata maombi kutoka kwa mkuu wa mkoa waliamua kutoa ardhi hiyo ili kusaidia juhudi za serikali za kuwa na viwanda.

“Tulipokea ombi na tumeamua kutoa eneo hili ambalo naamini litasaidia katika juhudi hizi za ujenzi wa viwanda vidogo katika mkoa huu, tutaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha wanafikia lengo,”alisema Iqbal.

Lakini katika mkutano wake na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Lukuvi alisema eneo hilo ni la serikali na kwamba wizara yake itamshughulikia mfanyabiashara huyo kwa kumdanganya mkuu wa mkoa.

Lukuvi alisema mfanyabiashara huyo aliidanganya serikali pamoja na kumdanganya mkuu wa mkoa Makonda ambaye ndiye aliyekabidhiwa eneo hilo kwa niaba ya serikali. Mbali na kosa la kuidanganya serikali, Lukuvi pia amesema atamchukulia hatua mfanyabiashara huyo kwa kumiliki ardhi kinyume cha sheria.

Alisema tayari amekwishafanya mawasiliano na mkuu huyo wa mkoa na kumuelewesha kuwa alidanganywa kwa kuambiwa kuwa anapewa eneo kwa ajili ya viwanda, huku eneo lenyewe likiwa ni mali ya serikali.

“Sitaki ardhi itumike kama sehemu ya wafanyabiashara kutakatishia fedha zao chafu,” alisema Lukuvi na kuwataka watu wote wanaomiliki maeneo mijini kujisalimisha kwa maofisa ardhi wa wilaya wa ajili ya uhakiki.

“Hilo eneo ni mali ya serikali, halijawahi kuwa mali ya mtu huyo aliyetajwa na kumkabidhi mkuu wa mkoa. Amemdanganya mkuu wa mkoa, na sisi hatukubali, tutamshughulikia kwa niaba ya mkuu wa mkoa,” alieleza Lukuvi, baada ya kuwapo madai ya wananchi kulalamika kuwa wameporwa ardhi yao.

Aidha, wizara hiyo imetayarisha hati 214 kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam waliosalimisha ofa zao za umiliki wa ardhi kwenye wizara hiyo ili wamiliki ardhi hizo kihalali.

Lukuvi alisema ni rahisi kwa wananchi wenye umiliki wa ofa kutapeliwa kuliko wakiwa na umiliki wenye hati ambazo ni halali hivyo ili kuondoa changamoto hiyo wizara ilitoa muda kwa wananchi kupeleka ofa hizo ili watayarishiwe hati halali.

“Kuwa na umiliki halali wa ardhi ni jambo kubwa kwa usalama wa wananchi wenyewe, nataka ifike siku Tanzania iwe haina mtu anayemiliki ardhi kwa kutumia ofa kwa sababu sasa hivi wizara haitoi ofa, ofa hizo zilishakoma siku nyingi,” alisema Lukuvi.

Aliongeza kuwa ingawa muda wa kusalimisha ofa hizo za umiliki umekwisha, lakini wizara hiyo inatoa muda zaidi kwa watu ambao bado hawajapeleka ofa zao katika halmashauri zao za wilaya kupeleka ofa hizo ili wamiliki ardhi hizo kwa hati.

Aidha, akizungumzia utayarishaji wa teknolojia itakayohusika na masuala yote ya ardhi inayojulikana kama ‘Mfumo Unganishi wa Ardhi’, Lukuvi alisema tayari Kampuni ya Kifaransa iliyoshinda zabuni inaendelea na kazi na Julai mosi mwaka huu hati ya kwanza ya kielektroniki ya mfano itatolewa.

Tayari jengo litakalotumika kwa ajili ya shughuli hizo limeshakamilika na mfumo huo bado unaendelea kutengenezwa ili kuwezesha wananchi wote wanaomiliki ardhi Tanzania wanamilikishwa hati za kielektroniki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post