RAIS MAGUFULI: VITA DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA SIYO YA KUFANYA KWA MZAHA WALA KUANGALIA MAJINA YA WATU AU VYEO VYAO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ameviagiza vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuhakikisha vinasimamia sheria ipasavyo ili kukabiliana na tatizo hilo hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 12 Februari, 2017 Ikulu Jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kuwaapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Rogers William Siyanga, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala, Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Joseph Edward Sokoine, Balozi wa Tanzania nchini Algeria Mhe. Omar Yusuf Mzee na Balozi wa Tanzania nchini Uganda Mhe. Grace Aaron Mgovano.
Mhe. Dkt. Magufuli amewataka viongozi wote wa Serikali kuungana na vyombo vya dola katika mapambano dhidi ya watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na ametaka mapambano hayo yasifanywe kwa mzaha wala kwa kuangalia majina ya watu, vyeo vyao na taasisi wanazoongoza.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza viongozi wote wa mikoa walioanza kukamata watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya na amewaomba Watanzania wote waunge mkono juhudi za kukabiliana na wanaofanya biashara na kutumia dawa za kulevya ambazo zinazidi kuangamiza nguvukazi ya Taifa.
“Niwaombe ndugu zangu tuungane katika vita hii dhidi ya dawa za kulevya, waandishi wa habari na wana mitandao tuweke mbele Utanzania wetu, akitokea mtu anapambana na dawa za kulevya tumuunge mkono badala ya kumchafua.
“Vita hii ni kubwa hatuwezi kwenda nayo kwa mzaha na Serikali itahakikisha inasimamia sheria namba 5 ya mwaka 2015 iliyohusu kuzuia na kupambana na dawa za kulevya ambayo ilitungwa na Bunge la 10 lililoongozwa na Spika Anna Makinda na sheria hiyo ikatiwa saini na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, nawapongeza sana kwa kutunga sheria hii.” Amesisitiza Mhe. Rais Magufuli
Pia, Mhe. Dkt. Magufuli amesema takwimu zinaonesha kuna watanzania 1,007 wamekamatwa na kufungwa gerezani katika nchi mbalimbali baada ya kupatikana na makosa ya kujihusisha na dawa za kulevya, na amemuagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mabalozi wote wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi hizo kutojihusisha kuwatetea waliofungwa kwa makosa hayo na badala yake waache sheria za nchi husika zichukue mkondo wake.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala kufanya mabadiliko makubwa ndani ya Idara ya Uhamiaji nchini kutokana na utendaji wake kutoridhisha.
“Nataka ukafanye mabadiliko makubwa (Total Reform), nataka Uhamiaji izalishe fedha kwa ajili ya nchi hii, nataka ukadhibiti utoaji hati za kusafiria (Passports) maana zimekuwa zikitolewa hovyohovyo” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao pamoja na kula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela, imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Kaimu Jaji Mkuu Mhe. Prof. Ibrahim Juma, Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali na Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Februari, 2017

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post