MWENDESHA BODABODA AFARIKI KWA KUGONGWA GARI AKIWAKIMBIA ASKARI WA USALAMA BARABARANI SHINYANGA

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro
*****
Kijana aliyejulikana kwa jina la Boaz William amefariki dunia kwa kugongwa gari wakati akidaiwa kuwakimbia askari wa usalama barabarani mjini Shinyanga.

Inaelezwa kuwa kijana huyo amefariki dunia Februari 13,2017 mchana wakati akijaribu kuwakimbia askari wa usalama barabarani waliomtaka asimame kutokana na makosa ya barabarani.

Askari wanaodaiwa kusababisha kifo hicho ni miongoni mwa askari ambao wamekuwa wakitapakaa mjini Shinyanga wakiwa na fimbo kisha kukamata waendesha bodaboda na wakati mwingine kuwachapa fimbo.

Kutokana na waendesha bodaboda kukusanyika na kutaka kufanya vurugu,Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro amelazimika kukutana na waendesha bodaboda hao ambao walionesha kuwa na hasira na kufanya nao kikao akiwasihi wasifanye vurugu.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya uhakika vya Malunde1 blog,mwili wa marehemu umesafirishwa kwenda mkoani Kigoma kwa ajili ya mazishi usiku wa kuamkia Februari 14,2017.

Inaelezwa kuwa ndugu wa marehemu walikubaliana mwili wa marehemu usafirishwe usiku huo licha ya jeshi la polisi kuwakataza kwa ajili ya mambo ya kiusalama lakini baada ya mwili wa marehemu kufanyiwa uchunguzi wa daktari jeshi la polisi liliwaruhusu kusafirisha mwili huo.

Hata hivyo maamuzi ya ndugu hao wa marehemu hayawakuridhisha baadhi ya waendesha bodaboda hao wakitaka mwili wa marehemu uagwe siku ya Jumanne Februari 14,2017 ingawa ndugu hao walidai kutokana na umbali kutoka Shinyanga kwenda Kigoma walisema ni vyema wakaanza safari usiku huo ili kufanya mazishi mapema ndipo uongozi wa chama cha waendesha bodaboda wakakubali mwii huo usafirishwe usiku huo.

Malunde1 blog imemtafuta kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro kuzungumzia malalamiko ya baadhi ya wananchi wakidai kuwa polisi ndiyo wamesafirisha mwili huo wa marehemu,haya ndiyo majibu yake:

"Tusafirishe mwili wa marehemu ili iweje? kwanza marehemu hakuwa anakimbizwa na askari,kilichotokea ni kwamba mwendesha bodaboda huyo aliambiwa asimame lakini akakaidi na kuendelea na safari yake huku amebeba abiria,wakati anaendelea ndipo akakutana na askari wengine ambao walikuwa wanaendelea na shughuli zao,yule mwendesha bodaboda akaanza kuwakwepa akidhani pengine wanaweza kumkamata ndipo akagonga gari lililokuwa linapaki",-anasema kamanda Muliro.

" Baada ya kutokea kwa tukio hilo nilikutana na waendesha bodaboda,jioni ndugu wa marehemu wakaomba wasafirishe mwili wa marehemu,tuliwazuia kwa sababu mwili wa marehemu ulikuwa haujafanyiwa postmortem kutokana na daktari kutokuwepo hospitali,lakini baadaye walitoa taarifa kuwa daktari amepatikana ndipo nikatoa askari kwenda kusimamia zoezi hilo huku ndugu wa marehemu akiwa hapo,baada ya kumaliza kufanya postmortem wakaomba kusafirisha mwili wa marehemu"-anaeleza kamanda Muliro.

"Mwili ukishafanyiwa uchunguzi sisi hatuna mamlaka ya kuzuia usizikwe,walipong'ang'ania kuchukua mwili ili wasafirishe,tukawaruhusu na wala hatukutoa gari yetu,walitumia gari ambayo ndugu wa marehemu walikodi,lakini kundi dogo la waendesha bodaboda walitaka mwili usisafirishwe usiku huo",ameongeza kamanda Muliro.

Kamanda Muliro amesema mwendesha bodaboda huyo alifanya makosa kukimbia askari polisi kwani alipaswa kusimama kwa mujibu wa sheria za usalama barabarani.

Kuhusu askari polisi kudaiwa kuwachapa fimbo waendesha bodaboda,Kamanda Muliro amesema askari wanaopaswa kuwa na fimbo ni wale wenye mamlaka na kama kuna askari anakuwa na fimbo na kuchapa raia ni kosa kisheria.

Mwenyekiti wa chama cha waendesha bodaboda manispaa ya Shinyanga Jacob Paul amesema chanzo cha kifo ni askari polisi wawili walikuwa wanamfukuza mwendesha bodaboda huyo na kusababisha agongwe gari na kufariki dunia akipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga.

"Baada ya mazingira,ndugu wa marehemu aliomba mwili wa marehemu usafirishwe kutokana na ndugu waliopo Kigoma wakiomba mwili wa marehemu usilale Shinyanga usafirishwe usiku huo kwani pesa kwa ajili ya kusafirisha mwili huo,ndipo nikawasiliana na kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ili mwili ufanyiwe postmortem na usafirishwe usiku huo ndipo kibali kikatolewa na mwili kusafirishwa majira ya saa tano na nusu usiku wa Februari"-anasema mwenyekiti huyo.

Hata hivyo inaelezwa kuwa huenda marehemu alikuwa na msongo wa mawazo wakati akiendesha pikipiki hiyo kutokana na misiba ambayo ameipata hivi karibuni baada ya kufiwa na mtoto na mke wake.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post