MLINZI AHUKUMIWA JELA MIAKA MIWILI KWA KUUA MCHIMBAJI MGODI WA MWADUI


Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga imemhukumu kutumikia jela miaka miwili aliyekuwa mlinzi wa kampuni ya ulinzi ya Zeneth Juma Masanja (35) baada ya kupatikana na kosa la kuua bila kukusudia.

Hukumu hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Jaji wa mahakama hiyo Victoria Makani baada ya kuridhika ya maelezo yaliyotolewa na pande zote mbili za mashtaka na utetezi na mshtakiwa kukubali kutenda kosa hilo.

Awali wakili wa serikali mkuu mfawidhi mkoa wa Shinyanga Pendo Makondo alieleza mahakama hiyo kuwa Septemba 24,2014 akiwa bunduki aina ya Shortgun alifyatua risasi nne hewani na kumpiga risasi Vene Edward (28) mkazi wa Maganzo wilayani Kishapu.

Akielezea zaidi wakili huyo alisema siku hiyo mshtakiwa akiwa na walinzi wenzake katika mgodi wa almasi wa Williamson ulioko Mwadui wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, waliona kundi la watu waliovamia eneo la mgodi huo na kuanza kuchimba mchanga unaodaiwa kuwa na madini hayo, wakaenda kuwafukuza ambako walianza kushambuliwa kwa silaha za jadi.

“Walipokwenda kwenye kundi hilo,walitoa amri ya kuwataka kusimame lakini kundi lile la watu walikimbia huku wakiwarushia walinzi hao mawe kwa mikono na makombeo, mishale na vipande vya nondo ambapo mshtakiwa Vene Edrward aliamua kufyatua risasi hewani mara nne na ndipo zilipompata marehemu tumboni, kiunoni mkono wa kushoto”, alisema.

Makondo aliongeza Vene Edward alipelekwa kituo cha polisi Maganzo kwa ajili ya fomu namba tatu (PF 3) kisha kupelekwa katika hospitali ya Kolandoto kwa ajili ya matibabu,Septemba 25,2014 mgonjwa aliandika maelezo akiwa wodini kuhusu tukio la kupigwa risasi na askari na alifariki dunia Septemba 28,2014 baada ya hali yake kubadilika.

Mshtakiwa Juma Masanja alikiri kutenda kosa hilo na kukubaliana na maelezo hayo ya wakili wa serikali.

Naye Wakili wa upande wa mshtakiwa Audax Costantine kutokana na mshtakiwa kukiri kutenda kosa na kutoisumbua mahakama na kuipotezea muda aliiomba mahakama impunguzie adhabu mshtakiwa kutokana na kwamba bado ni kijana na anategemewa na familia yake kwani ana mke mmoja na watoto watano.

Hata hivyo Jaji wa mahakama hiyo Victoria Makani baada ya kuridhika na utetezi wa pande zote mbili alimtia hatiani mshtakiwa kwa kuua bila kukusudia na kwamba atatumia kifungo cha miaka miwili jela.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post