MAKONDA ATAJA WASANII WENGINE WANAODAIWA KUJIHUSISHA NA MADAWAYA KULEVYA...YUMO VANESA MDEE


SIKU moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutangaza vita dhidi ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, makubwa zaidi yamezidi kujitokeza baada ya orodha ya watu hao wanaojihusisha na biashara hiyo haramu kuongezeka.

Mkuu huyo wa mkoa amemuagiza Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro kuwaongeza askari wengine watatu katika orodha ya watuhumiwa hao ambao alidai katika wiki mbili zilizopita walipewa Sh bilioni moja kutokana na biashara hiyo.

Aliwataja askari hao kuwa ni Muddy Zungu, Fadhili na Ben huku wengine wanaopaswa kuongezwa katika orodha hiyo ni pamoja na msanii Vanesa Mdee na Video Queen, Tunda Sebastian.

Aidha, Makonda alimuagiza Sirro kuhakikisha wasanii na watu wengine walioko kwenye orodha aliyoitaja awali ambao hawakufika, wakamatwe mara moja na wawekwe ndani hadi Jumatatu kwa ajili ya mahojiano.

“Hawa nataka waunganishwe na wale wenzao, hatuwezi kuwa na watumishi wanaochafua taaswira ya jeshi la polisi na nimepata taarifa mmoja amenunua nyumba Kigamboni,” alisema Makonda.

Makonda pia alimtaja mtu mwingine ambaye ni mfanyabiashara mkubwa wa dawa hizo, Omari Sanga kuwa ni mmoja kati wa watu waliosababisha asilimia 65 hadi 70 ya Watanzania waishie kwenye jela nchini China.

Pia aliitaja hoteli ya Meditteranian iliyopo Kawe kuwa nayo ni miongoni mwa hoteli ambazo zimekuwa zikifanya biashara hiyo kinyume na leseni waliyopewa.

Watuhumiwa waliofika ni pamoja na aliyewahi kuwa Miss Tanzania, Wema Sepetu, Khaleed Mohammed (TID), Hamidu Chambuso (Dogo Hamidu/ Nyandu Tozzy) pamoja na Babuu wa Kitaa.
IMEANDIKWA NA KATUMA MASAMBA wa gazeti la habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post