MNYAMA SIMBA ACHINJWA USIKU ZANZIBAR, AZAM FC BINGWA MAPINDUZI


Himid Mao
Klabu ya Azam ya jijini Dar es Salaam imetwaa ubingwa wa kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga Simba SC ambayo pia ni ya jijini Dar es salaam kwa bao 1-0. 

Bao la kipindi cha kwanza lililofungwa na Himid Mao liliiwezesha Azam FC kutwaa kwa mara ya tatu taji la Mapinduzi, baada ya kuifunga Simba kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar.

Kwa ushindi huo, Azam FC sasa imeifikia rekodi ya Simba ya kushinda taji hilo mara ya tatu.

Simba walifuzu kucheza fainali hiyo baada ya kuwafunga watani zao Yanga kwa penalti 4-2 katika mchezo wa nusu fainali, huku Azam wenyewe wakiwatoa Taifa Jang’ombe katika hatua hiyo kwa kuifunga bao 1-0.

Azam FC waliandika bao hilo pekee katika dakika ya 13 kupitia kwa mchezaji huyo, ambalo lilidumu hadi dakika 90 za mwisho.

Awali, katika dakika za mapema Simba walilifikia mara mbili lango la Azam lakini walishindwa kutumbukiza mpira wavuni kwa wapinzani wao.

Shizza Kichuya alipoteza nafasi ya wazi ya kufunga bao katika dakika ya 39 baada ya kubaki yeye na lango baada ya kipa wa Azam FC Aishi Manula kumtemea mpira, lakini alishindwa kuujaza wavuni.

Katika mchezo huo Himid Mao wa Azam alioneshwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Jamvier Bukungu.

Aggrey Moris ndiye alikuwa mchezaji bora katika fainali hiyo iliyohudhuriwa na watazamaji kibao.

Vikosi:
Azam FC:Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Aggrey Morris, Yakubu Mohamed, Stephan Kingue, Salum Abubakar, Himid Mao, John Boko, Yahaya Mohamed na Joseph Mahundi.

Simba:Daniel Agyei, Besala Bukungu, Mohamed Hussein, James Kotei, Method Mwanjali, Shiza Kichuya, Juma Luizio, Mzamiru Yassin/Pastory Athanas na Mwinyi Kazimoto/Laudit Mavugo (dk 42).
IMEANDIKWA NA MOHAMED AKIDA wa gazeti la habarileo ZANZIBAR

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post