RAIS MAGUFULI AZUIA SERIKALI KUPELEKA CHAKULA CHA MSAADA MISENYI

Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli amezuia serikali kupeleka chakula cha msaada wilayani Misenyi mkoani Kagera kwa madai kuwa wilaya hiyo haina sababu ya kukumbwa na tatizo la njaa.


Rais Magufuli amekataa serikali kupeleka chakula cha msaada katika wilaya hiyo na kusema haikubaliki kwa eneo hilo lenye mvua za kutosha na hali nzuri ya kilimo na kwamba haiwezekani kulia njaa wakati kuna uwezekano wa kuzalisha kwa ajili ya chakula.


Amesema hayo wakati akiweka jiwe la msingi katika kituo cha afya cha kata ya Ishozi Wilayani Misenyi Mkoani Kagera ambapo yupo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani humo kukagua maendeleo mbalimbali.


Katika hatua nyingine Rais Magufuli, amesema kuwa serikali haitaweza kujenga makazi ya kila mwathirika wa tetemeko mkoani Kagera kwa kuwa ina jukumu la kujenga miundombinu itakayokuwa na manufaa kwa jamii nzima kama Zahanati, Shule na barabara.


Amesema kuwa kuna baadhi ya watu ambao nyumba zao hazikuharibika kiasi kikubwa lakini wakadanganywa na baadhi ya watu kuwa watajengewa hivyo wakazibomoa kwa kutaka kujengewa nyumba mpya.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipiga makofi mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika Kituo cha Afya cha Kabyaile Misenyi Mkoani Kagera.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikagua maeneo ya ujenzi wa kituo hicho cha Afya cha Kabyaile kilichopo Misenyi mkoani Kagera.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi katika eneo la mradi wa ujenzi wa kituo hicho cha Afya cha Kabyaile kilichopo Misenyi mkoani Kagera.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post