Picha 40: MKE AUAWA KWA KUPIGWA NA MME WAKE KISA KACHUMBARI ILIYOCHACHA,ASKOFU WA KANISA KATOLIKI SHINYANGA AFUNGUKA
Mwanamke aliyejulikana kwa jina la Stella Apinius (39) mkazi wa mtaa wa Mageuzi kata ya Ngokolo manispaa ya Shinyanga ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na mme wake Ibrahim Daniel (42) kwa kile kilichodaiwa kuwa amepewa kachumbari iliyochacha.Mwandishi mkuu wa Malunde1 blog,Kadama Malunde,anaripoti.Tukio hilo limetokea juzi Januari 17,2017 usiku baada mwanamme huyo kumshushia kipigo mke wake wa ndoa  akidai kuonyeshwa kachumbari ambayo haikuhifadhiwa vizuri na kupatiwa mboga nyingine aliyodai haina kiwango.Inaelezwa kuwa mwanamme huyo alifika nyumbani akiwa amelewa kisha kuulizia kuhusu kachumbari ambayo alikula jana yake ndipo mtoto aliyekuwa akimlea aliyefahamika kwa jina la Elizabeth akamuonesha kachumbari hiyo ambayo tayari ilikuwa imechacha.


Akisimulia mkasa huo, mtoto wa marehemu aliyefahamika kwa jina la Daniel Ibrahim (12) anayesoma darasa la sita katika shule ya msingi Mwadui katika manispaa ya Shinyanga,alisema baba yake alifika nyumbani saa moja usiku ,alimkuta yeye akiwa na mtoto mwenzie Elizabeth (13) ndipo baba huyo alipoanza kumhoji Elizabeth kuwa kwanini kachumbari imeharibika.

“Baada ya kuingia ndani baba alimuuliza Eliza kuwa kachumbari aliyoiacha tarehe 16/1/2017 iko wapi,akaoneshwa baada ya kuiangalia aliiona imechacha na kuonekana na uchafu, ndipo alitoka nje na kuchukua fimbo ambayo huwa anaiweka juu ya nyumba na kutaka kuanza kumpiga lakini kabla ya kumpiga Eliza alichoropoka na kukimbia nje”,alieleza Daniel .

“Baada ya Eliza kukimbia,mama ambaye alikuwa kazini alifika nyumbani, akamkuta baba akifoka, akauliza kuna nini?,baba akasema kwa nini hakupika mboga yenye kiwango na kwanini mlipika ugali mwingine wakati kulikuwa na ugali uliobaki mchana?”,alieleza mtoto huyo.

Aliongeza kuwa kufuatia maswali hayo mama huyo alimjibu mme wake kwa hasira kuwa kwanini hakuacha pesa nyumbani ili wanunue mboga yenye kiwango anachotaka yeye majibu ambayo yalimkera baba huyo na kuanza kumshushia kichapo mke wake.

“Mama alipofika nyumbani baba aliendelea kufoka ndipo mama alimjibu kwa hasira kwanini hukuacha fedha ya matumizi ya kuweza kupika mboga yenye kiwango?,ndipo alianza kumpiga kwa kikombe na mateke, akaanguka ndipo nilikimbia kwa kuwataarifu majirani walikuja na kukuta mama ameanguka chini ” alifafanua Daniel.

Baadhi ya majirani waliofika katika tukio hilo, Gloria Shija na Leticia Mashala,walisema walipofika walikuta mlango umefungwa wakaanza kumgongea ili afungue, alikataa na kusema ana kazi kidogo anaifanya wasubiri,walichungulia dirishani wakamuona anampuliza puani na masikioni huku akimmwagia maji ili azinduke,baada ya kuona hazinduki ndipo alifungua mlango.

Shija alisema waliingia ndani na kumkuta akiwa amemkalisha chini huku akiwa ameinamisha shingo ambapo walimbeba na kumtoa nje na kujaribu kummwagia maji tena lakini ilishindikana ndipo walichukua uamuzi wa kumpeleka hospitalini walifika na kuanza kupimwa lakini alionekana tayari ameshafariki muda mrefu.

Naye Shangazi wa marehemu Getruda Vitalis alisema wanandoa hao wamekuwa wakigombana mara mara kwa mara,na wamewahi wamesuluhishwa mpaka kanisani walikofungia ndoa yao tarehe 14.04.2009.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Mageuzi Emmanuel Joshua Sama chanzo cha mauaji hayo ni kachumbari iliyochacha iliyokuwa imetunzwa vibaya na mtoto waliokuwa wakimlea Elizabeth na mama alipoingilia ugomvi huo ndipo akashushiwa kipigo.

“Baada ya baba anayedaiwa kuwa alikuwa amelewa kudai kachumbari yake,ndipo mama aliingilia kati na mwanamme huyo kumgeuzia kibao,vipimo vya daktari vinaonesha marehemu alipigwa na kitu kizito kwenye utosi kichwa kikavimba damu ikavujiandani na alikuwa na michubuko mikononi”,alieleza Mwenyekiti wa mtaa.

Akizungumza wakati wa misa ya wafu iliyofanyika leo jioni katika kanisa la Mama Mwenye Huruma lililopo Ngokolo Mjini Shinyanga,Askofu wa kanisa katoliki jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu alieleza kusikitishwa na mauaji hayo na kutaka kitendo kama hicho kisijirudie tena katika familia.

"Hili tukio ni baya,linasikitisha,lisijirudie tena katika familia zetu",alisema kwa ufupi.

 Msemaji wa familia ya marehemu Baraka Majigwa alisema tukio hilo limetokana na uzembe wa akina mama kutopaza sauti zao kutokana na ukatili wanaofanyiwa na waume zao.

"Tukio hili litufumbue macho akina baba na akina mama,akina baba acheni kuwafanyia ukatili wake zenu,nanyi akina mama acheni kunyamaza mnapofanyiwa ukatili,naomba pia serikali za mitaa ziwe na kumbukumbu ya majina ya wanawake wanaofanyiwa ukatili",alieleza Majigwa.

Kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Elias Mwita alisema mtuhumiwa wa mauaji hayo Ibrahim Daniel anashikiliwa na jeshi hilo na baada ya marehemu kuchunguzwa alionekana kuwa na jeraha katikati ya kichwa chake.

Mwita alisema uchunguzi wa awali inasemekana chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi wa kifamilia ambao ulikuwa unamhusu Elizabeth ambaye walikuwa wakimlea kutoka mwaka 2016 na wanaendelea kufanya uchunguzi zaidi kuhusu kifo hicho.

Mwili wa marehemu umesafirishwa kupelekwa wilayani Ngara mkoani Kagera kwa ajili ya mazishi.

Inaelezwa kuwa ukatili dhidi ya wanawake katika mtaa huo wa Mageuzi umekithiri ambapo hivi karibuni mwanamke mwingine alifariki dunia baada ya kupigwa na mme wake.

 Mwandishi Mkuu wa Malunde1 blog,Kadama Malunde alikuwepo eneo la tukio ametuletea Picha 40...Tazama hapa chini
Ndani ya kanisa la Mama Mwenye Huruma lililopo Ngokolo Mjini Shinyanga,Askofu wa kanisa katoliki jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu akiongoza misa ya wafu kwa ajili ya kumwombea marehemu Stella Apinius
Picha ya marehemu Stella Apinius ikiwa kwenye jeneza
Misa inaendelea
Misa inaendelea
Misa inaendelea
Waumini wakiwa kanisani
Askofu Sangu akimwombea marehemu Stella Apinius
Askofu Sangu akimwombea marehemu

Waumini,ndugu wa marehemu na watu mbalimbali wenye mapenzi mema wakiwa kanisani

Wanakwaya wakiwa kanisani


Masisita wakiaga mwili wa marehemu


Ndugu,jamaa na marafiki wakiaga mwili wa marehemu


Misa inaendelea

Zoezi la kuaga mwili wa marehemu kanisani likiendelea
Wanakwaya wakiaga mwili wa marehemu
Mtoto Elizabeth aliyekuwa analelewa katika familia ya marehemu.
Ndugu wa marehemu wakiaga mwili wa mpendwa wao
Askofu Liberatus Sangu akizungumza wakati wa misa ya kuombea wafu 
Askofu Sangu aliiasa jamii kuachana vitendo viovu na kutaka tukio kama hilo la mauaji lisijirudie tena katika familia
Askofu Sangu akimwombea marehemu
Askofu Sangu akiomba kanisani
Mwili wa marehemu ukitolewa kanisani
Mwili ukiwa nje ya kanisa 
Mwili wa marehemu ukiwa kwenye gari kwa ajili ya kupelekwa nyumbani kwake mtaa wa Mageuzi kata ya Ngokolo katika manispaa ya Shinyanga
Mamia ya wakazi wa Shinyanga wakiwa nje ya kanisa 
Mwili wa marehemu ukiingizwa ndani ya nyumba ya marehemu katika mtaa wa Mageuzi kata ya Ngokolo
Waombolezaji wakiwa nyumbani kwa marehemu
Wakazi wa Mtaa wa Mageuzi wakiwa nyumbani kwa marehemu
Wakazi wa mtaa wa Mageuzi wakiaga mwili wa marehemu 
Zoezi la kuaga mwili wa marehemu likiendelea nyumbani
Mtoto wa marehemu Daniel Ibrahim(mwenye nguo nyeusi) akiwa na ndugu zake msibai

Kulia ni Balozi wa Ubalozi wa Mageuzi Juu,Samwel Shija Ng'hwaya akizungumza msibani
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Thoma Mtume John Kapelembe akitoa salamu za rambirambi
Mwenyekiti wa mtaa wa Mageuzi Emmanuel Joshua akizungumza msibani
Mwenyekiti wa mtaa Emmanuel Joshua akizungumza
Msemaji wa familia Baraka  Majigwa akizungumza
Kulia ni rafiki yake na marehemu Maria Lusambo ambaye ameachiwa jukumu la kuangalia nyumba ya marehemu akiteta jambo na shangazi yake na marehemu Getruda Vitalis
Mwenyekiti wa mtaa wa Dome katika kata ya Ndembezi Solomoni Naringa Najulwa akielezea namna mtoto Eliza(aliyemshika) alivyoanza kulelewa na marehemu baada ya kukosekana wazazi wake na sasa mlezi wake amefariki

Mwenyekiti wa mtaa wa Dome katika kata ya Ndembezi Solomoni Naringa Najulwa aliwashukuru ndugu wa marehemu kukubali kumlea mtoto Eliza na kama watashindwa basi waitarifu serikali ili iweze kumlea mtoto huyo.
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post