MKULIMA MWINGINE AJERUHIWA KILOSA,AKATWA KATWA NA SIME KICHWANI


MTU mmoja mkazi wa Kijiji cha Mamoyo, Kata ya Mabwerebwere, Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro, Omary Sululu (52), amenusurika kifo baada ya kukatwakatwa na sime kichwani na watu wanaodaiwa kuwa ni wafugaji.

Taarifa zilizopatikana kijijini hapo, zinasema Sululu alijeruhiwa na wafugaji hao wakati alipokuwa akizuia mifugo isile mazao katika shamba lake.

Tukio hilo limetokea siku chache baada ya Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Joshua Lugaso, kutoa tamko la kulaani matukio ya kikatili yanayofanywa na wafugaji dhidi ya wakulima wilayani Kilosa.

Akizungumza na MTANZANIA akiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, Sululu alisema alijeruhiwa Januari mosi, saa za mchana wakati alipokuwa katika shamba lake la mahindi na migomba.

“Nilipokuwa shambani, niliona kundi la ng’ombe likiingia shambani kwangu na nilipokuwa katika harakati za kuwafukuza mifugo hao, wafugaji watatu walitokea kichakani wakiwa na marungu, sime na fimbo.

“Waliponikaribia, walinitaka niiache mifugo iendelee kula mazao yangu kwa sababu ilikuwa na njaa. Wakati nikijibizana nao, mifugo hiyo ilikuwa inaendelea kula mazao yangu.

“Baadaye walijitokeza wafugaji wanane wakiwa na silaha mbalimbali na kunihoji kwanini ninazuia mifugo isile chakula.

“Kisha walinizunguka wakaanza kunipiga na marungu kichwani, walinikata na sime kichwani na kuniangusha wakati nimepoteza fahamu.

“Walipoona nimeanguka chini, walikimbia na mifugo yao, lakini baada ya kama dakika 15 hivi alitokea dereva wa pikipiki ambaye aliniinua na kunipeleka hadi kituo cha polisi,” alisema Sululu.

Kaimu Mganga Msaidizi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilosa, Thomas Kibula, alithibitisha kumpokea Sululu hospitalini hapo akiwa na majeraha kichwani.
Na RAMADHAN LIBENANGA- MTANZANIA KILOSA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post