Picha: MGODI WA BUZWAGI WAZINDUA KAMPENI YA WAKIA MOJA MTI MMOJA,MITI MILIONI 1.6 KUPANDWA KAHAMAMkuu wa wilaya Kahama Fadhili Nkurlu akipanda mti kuashiria uzinduzi rasmi wa kampeni ya upandaji miti milioni moja na laki sita itakayopandwa katika maeneneo mbalimbali wilayani kahama kwa lengo la kutunza mazingira pamoja na kuufanya mji wa Kahama upendeze.
Mkuu wa wilaya kahama Fadhili Nkurlu akimwagia maji mti alioupanda wakati alipozindua kampeni ya upandaji miti
Mkuu wa polisi wilaya ya Kahama Mussa Mchenya akishiriki pia upandaji miti.
Afisa Usalama wa Wilaya ya Kahama Aretus Lyimo akishiriki upandaji miti wakati wa zoezi la uzindunzi wa upandaji miti milioni moja na laki sita.
Katibu Tawala wa Wilaya Kahama Timothy Ndanya akishiriki pia kupanda miti.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Asa Mwaipopo akifurahia wakati alipokuwa akipanda mti katika eneo la mgodi wa Buzwagi.
Meneja raslimali watu wa Mgodi wa Buzwagi Solomon Rwangabwoba akifurahia kupanda mti wakati wa uzindunzi wa kampeni ya upandaji miti milioni moja na laki sita itakayoendeshwa na mgodi wa Buzwagi.

******************************************************
PICHA ZA MAAFISA WAKUU WA KAMPUNI YA ACACIA MINING PLC WAKIPANDA MITI WAKATI WALIPOFANYA ZIARA KATIKA MGODI WA BUZWAGI.
Afisa Mkuu Mwendeshaji wa Kampuni ya Acacia Mark Marcombe akishiriki zoezi la upandaji miti milioni moja na laki sita miti ambayo inatajwa kuwa itasaidia katika kuipendezesha wilaya ya Kahama.
Afisa Mkuu wa Idara ya Raslimali watu wa Kampuni ya Acacia Peter Gereta akishiriki zoezi la upandaji miti.
Makamu wa Rais wa Kampuni ya Acacia anaeshughulikia Masuala ya Kampuni (Corporate Affairs) Deo Mwanyika akishiriki pia kupata mti.
Mh. Salome Makamba MB-(Viti Maalumu) akishiriki pia upandaji miti baada ya kupita karibu na eneo ambapo zoezi la upandaji miti lilikuwa likifanyika na akaona ni vyema na yeye akashiri katika kuunga mkono jitihada za Mgodi wa Buzwagi katika kupanda miti itakayosaidia katika utunzaji wa mazingira wa wilaya ya Kahama na Taifa kwa ujumla.
Afisa Mkuu wa Idara ya Utafiti wa madini (Exploration) Peter Spora akifurahia wakati alipokuwa akipanda mti katika eneo la Mgodi wa Buzwagi.Taarifa kwa vyombo vya Habari:
Wakia Moja Mti Mmoja - Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi wajipanga kupanda miti milioni 1.6
Kahama: 31/01/2017. Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi leo umezindua kampeni ya upandaji miti katika Wilaya ya Kahama ikiwa na lengo la kupanda mti kwa kila wakia ya dhahabu ambayo imechimbwa kwenye mgodi wa Buzwagi, ambapo miti zaidi ya milioni moja na laki sita inatarajiwa kupandwa katika kipindi cha miaka miwili.
Akizindua kampeni hiyo Mkuu wa wilaya ya Kahama Fadhili Nkurlu ameupongeza uongozi wa Mgodi wa Buzwagi kwa hatua hiyo na kusema ni ya kizalendo kwa kuwa itasaidia katika kuboresha hali ya mazingira ya wilaya ya Kahama.
“Jukumu la upandaji miti na kuhakikisha mazingira yetu yanatunzwa ni letu sote, Wenzetu wa Buzwagi wameanza kuonyesha jitihada kwa kupanda miti milioni moja na laki sita, hivyo sote kama Jamii hatuna budi kuwaunga mkono kwa kuhakikisha kila mmoja wetu katika eneo lake anapanda miti na kuifanya wilaya yetu ya Kahama izidi kupendeza”Alisema Nkurlu.
Akizungumzia Malengo ya Kampeni hiyo Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Asa Mwaipopo amesema kama wadau muhimu wa mazingira wanalojukumu la moja kwa moja kuhakikisha shughuli za utunzaji wa mazingira zinakuwa ni sehemu ya maisha ya kila siku.
Na kupitia mipango ya muda mrefu uongozi umejiwekea lengo la kupanda mti mmoja kwa kila wakia moja ya dhahabu itakayokuwa ikizalishwa katika kipindi chote cha uhai wa Mgodi wa Buzwagi ambapo inakisiwa mpaka shughuli za uzalishaji zitakapositishwa takribani wakia milioni moja na laki sita zitakuwa zimezalishwa.
“Leo tunazindua awamu ya kwanza ya kampeni hii ambayo itahusisha upandaji wa miti laki tano, ambapo mpaka sasa miti elfu ishirini imekwisha pandwa na tunatarajia mpaka mwisho wa mwaka huu awamu ya kwanza ya miti laki tano itakuwa imepandwa” Alisema Mwaipopo. “
“Kwa kupanda miti hii, tunakusudia kuwa sehemu muhimu ya wadau wa mazingira wenye lengo la kuipendezesha wilaya yetu ya Kahama, pia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na kuonyesha utayari wetu kama Kampuni katika kurejesha katika hali ya awali ya mazingira ya eneo la Mgodi itakapofikia wakati wa kuufunga. Aliongeza Mwaipopo.
Miti aina mbalimbali inatarajiwa kupandwa katika zoezi hili huku mti maarufu wa “Acacia” unaobeba jina la Kampuni mama ya Acacia Mining Plc inayomiliki Mgodi wa Buzwagi ikiwa ni sehemu ya miti itakayopandwa,
Huku zaidi ya shilingi milioni mia sita na arobaini na tano zikitarajiwa kutumika katika awamu ya kwanza ya upandaji miti laki tano.
Katika hatua nyingine maafisa wakuu wa Kampuni ya Acacia kutoka ofisi za Acacia Mining Plc London pamoja na Dar es salaam walishiriki pia katika zoezi la upandaji miti katika eneo la Mgodi wa Buzwagi wakati walipofanya ziara ya kikazi mgodini hapo.
“Wakia Moja Mti Mmoja”
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano Mgodi wa Buzwagi
Simu  +255 22 2164 200

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post