ALIYETUPA MTOTO MCHANGA KWENYE CHOO CHA KANISA SHINYANGA AKAMATWA

Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga linamshikilia binti aliyejulikana kwa jina la Neema Japhet (23) kwa tuhuma ya kumtupa mtoto  wa siku moja  kwenye choo cha kanisa la  Afrika Inland Church Tanzania  (AICT) la Kitangiri katika manispaa ya Shinyanga.
 
Kaimu kamanda wa jeshi la polisi mkoa  Elias Mwita alisema mwanamke huyo alikamatwa Januari 24,2017 majira ya saa tatu asubuhi na majirani zake chumbani kwake alipokuwa amepanga eneo la Kitangiri na kisha kutoa taarifa  polisi .
 
Mwita alisema jeshi la  polisi lilifika katika eneo hilo kisha kumkamata kwa tuhuma ya kumtupa mtoto wa siku moja chooni baada ya kujifungua  siku ya Ijumaa wiki iliyopita na  baada ya kuhojiwa alikiri kufanya kitendo hicho.
 
 “Baada ya mtu aliyetupa mtoto huyo kutojulikan, tulitoa wito kwa wananchi ili kushirikiana nasi ili kumbaini na juhudi za wananchi za kumsaka zimezaa matunda sasa majirani wameweza kumbaini mwanamke huyo  kuwa ndiye aliyehusika na unyama huo na amekiri kuhusika  na utupaji wa mtoto”,alisema Mwita.
 
Mwita alieleza kuwa mwanamke huyo alidai alikwenda chooni kwa lengo la kujisaidia lakini  ikatokea bahati mbaya  mtoto atumbukia kwenye tundu la choo.
 
Aliongeza kuwa  hivi sasa wanafanya utaratibu wa sheria  ili kumfikisha mahakamani ili kujibu tuhuma  hiyo.
 
Mwenyekiti  wa  mtaa wa  Kitangiri   Habiba  alisema mtoto huyo alitupwa chooni mnamo majira ya saa kumi na moja  jioni  tarehe  20/01/2017 ambapo baadhi ya waumini wa kanisa hilo walisikia sauti ya mtoto  mchanga ikitokea katika choo cha kanisa.
 
Jumanne alisema walichukua jukumu la kubomoa choo hicho na kumkuta mtoto akiwa hai kisha kumpeleka katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga ingawa hata hivyo mtoto huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu.
 Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post