MWANAFUNZI AFARIKI AKIOGELEA KWENYE BWAWA LA HOTELINB-Siyo bwawa la hoteli ya Mount Meru
MWANAFUNZI wa darasa la tano wa Shule ya Msingi Sekei iliyopo jijini Arusha, Cliff Laiza (12) amekufa wakati akiogelea kwenye bwawa lenye kina kirefu katika Hoteli ya Kitalii ya Mount Meru iliyopo jijini hapa katika sherehe ya Krismasi.

Tukio hilo ni la juzi majira ya saa 12 jioni wakati Cliff na watoto wengine, walipokuwa wakiogelea katika hoteli hiyo, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Krismasi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kaimu Meneja wa Hoteli ya Mount Meru , alithibitisha kutokea kwa kifo cha mwanafunzi huyo na kusema kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi na watatoa ufafanuzi baada ya polisi kukamilisha upelelezi wa tukio hilo.

Baadhi ya watoto waliokuwa wakiogelea na Cliff kwenye hoteli hiyo, walisema alihama ghafla kwenye bwawa la watoto na kwenda kuogelea bwawa linalotumiwa na watu wazima, ambalo wakati huo hapakuwa na mtu yeyote akiogelea, lakini ghafla hakuonekana tena hadi alipokutwa anaelea juu ya maji.

Babu wa mtoto huyo, Emanuel Meage alieleza kusikitishwa na tukio hilo na kueleza kuwa mjukuu wake aliaga kuwa anaenda kuogelea katika Hoteli ya Mount Meru yeye na wenzake. Hata hivyo, alisema alishangaa kusikia amekufa na kwa sasa wanamsubiri baba yake ili kujua ni hatua zipi wanazichukua kutokana na tukio hilo.

Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya wazazi waliutupia lawama uongozi wa hoteli hiyo kwa kushindwa kuwa na usimamizi mzuri na ulinzi wa watoto hao, badala yake wamekuwa wakijali kukusanya fedha na kuwaacha watoto wajiongoze, hatua ambayo si sahihi kwa vile eneo hilo ni hatari na si salama kwa mazingira ya watoto.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa polisi wapo kwenye uchunguzi na atalitolea ufafanuzi baada ya uchunguzi kukamilika.

Alisema hakuna mtu anayeshikiliwa kutokana na tukio hilo.
Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post