690 MBARONI KWA UHALIFU WA MTANDAO,WAMO MATAPELI,WEZI NA WAPORAJI WA SIMU ZA MKONONI


SERIKALI kupitia kitengo maalum cha uchunguzi wa jinai ya kimtandao, imefanikiwa kukamata watuhumiwa 690 kwa tuhuma za kufanya uhalifu wa mtandao.

Watuhumiwa hao ni matapeli, wezi, waporaji wa simu za mkononi na wengineo wanaotumia mfumo wa intaneti kuibia watu wasiokuwa na hatia.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projestus Rwegasira alisema juzi jioni kuwa ofisi yake imekuwa ikikabiliana kikamilifu na wahalifu hao.

Alisitiza kwamba wahusika wote wa vitendo hivyo, watakamatwa. Meja Jenerali Rwegasira alikuwa akizungumza katika mahojiano katika kipindi cha Tunatekeleza, kinachorushwa na Televisheni ya Taifa(TBC). Kwamba wizara yake kwa kushirikiana na vyombo vya serikali, inaandaa mashtaka dhidi ya watuhumiwa waliokamatwa na watafikishwa mahakamani.

“Tunafanya kila juhudi kuzuia vitendo vya uhalifu wa kimtandao, tayari tumekamata baadhi ya watuhumiwa na watakabiliana na mkono wa sheria mahakamani,” alisema.

Alisema serikali imeunda kitengo maalumu chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, kukabiliana na udanganyifu na uhalifu wa kimtandao nchini na kimekuwa kikifanya kazi nzuri.

Rwegasira alisema, “Ningependa kuutangazia umma kuwa huru kutoa taarifa ya vitendo kama hivyo polisi mara wanapoona, tuna uwezo wa kufuatilia simu zilizoibwa na kuwakamata watuhumiwa”.

Mwezi Januari mwaka huu, Mkuu wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Veronica Sudayi alisema tangu kupitishwa kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao na Miamala ya Kielektroniki ya 2015 mwezi Septemba 2015, kiwango cha wizi na udanganyifu nchini, kimepungua kwa asilimia 60.

Sudayi alisema hayo wakati akizungumza na wafanyakazi na wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kuhusu Sheria hiyo ya Makosa ya Mtandao. Kuhusu amani na usalama, katibu mkuu huyo alisema serikali imejiandaa vya kutosha kulinda watu na mali zao na kujipanga vya kutosha.

Alisema jeshi la polisi liliweza kukabiliana na changamoto za kiusalama katika mikoa ya Tanga na Mwanza baada ya watu wasiokuwa na hatia kuuawa na majambazi. Alisema katika tukio la Tanga, watuhumiwa 28 walikamatwa na wengine nane walikamatwa kuhusiana na tukio la Mwanza.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post